Baba Mtakatifu Fransisko, amempa hadhi ya Umonsinyori (The title of Chaplain of His Holiness) Mheshimiwa sana Padre Dominic Makalanga Mgata, wa Jimbo Katoliki Shinyanga.
Taarifa ya kupewa hadhi ya Umonsinyori kwa Padre Mgata ambaye kwa sasa anafanya utume wake katika Parokia ya Nyalikungu wilayani Maswa mkoani Simiyu, imetolewa leo Desemba 9, 2024 na Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu.
Askofu Sangu amewaalika Mapadre, watawa na waamini wote kuendelea kumwombea Monsinyori Dominic Makalanga Mgata kwa heshima hiyo aliyopewa na Kanisa, ili Mwenyezi Mungu azidi kumjalia afya njema na Baraka tele katika utumishi wake.
Umonsinyori ni hadhi ya heshima ya pekee ambayo Mapadre wachache hupewa na Baba Mtakatifu kwa mapendekezo ya Askofu wao wa Jimbo, kutokana na mchango mkubwa walioufanya katika utume wa Kanisa.
Jimbo Katoliki Shinyanga kwa sasa litakuwa na jumla ya Mapadre watatu wenye hadhi ya Umonsinyori waliopewa heshima hiyo chini ya uongozi wa Askofu Liberatus T.K. Sangu, ambao ni Monsinyori Nobert Ngusa anayefanya utume wake katika Parokia ya Shy bush, Monsinyori Martine Mhango (Mwanamilembe) anayefanya utume wake katika Parokia ya Buhangija na Monsinyori Dominic Makalanga Mgata anayefanya utume wake katika Parokia ya Nyalikungu Maswa.