Na Mapuli Kitina Misalaba
Polisi wa Kata ya Kambarage, Mkaguzi Msaidizi wa
Jeshi la Polisi (A/INSP) Happiness Mathias Madondola, ametoa wito kwa wazazi na
walezi kuhakikisha wanawalinda watoto dhidi ya ukatili wa kijinsia, hasa
kipindi hiki cha likizo za shule.
Ameyasema hayo kwenye kikao cha wazazi na wanafunzi
wa shule ya msingi Kambarage mjini Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine amesema
ni muhimu wazazi kuwajali watoto kwa kuwapatia mahitaji muhimu ya shule, lakini
pia kuimarisha ulinzi wao kwa kufuatilia wanaposhinda, wanacheza na nani, na
kuwapa kazi ndogo za nyumbani zinazowasaidia kujifunza majukumu ya kijamii.
Aidha, A/INSP Madondola amewaasa wazazi kuwa
waangalifu na wageni wanaolala nyumbani, akisisitiza kuwa hali si shwari.
“Hakikisha watoto unalala nao mama kama hakuna vyumba vya ziada,” amesisitiza,
akitahadharisha juu ya uwepo wa mjomba, babu, au baba wadogo na wakubwa ambao
huenda wakahatarisha usalama wa watoto.
Katika juhudi za kuhamasisha jamii kushirikiana na
vyombo vya usalama, A/INSP Madondola amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa za
wahalifu na uhalifu. “Tusiwe wasiri. Wahalifu tunao majumbani mwetu, tuwataje
ili hatua zichukuliwe,” amesema.
Mbali na wito huo, A/INSP Madondola ametoa msaada
kwa wanafunzi, ikiwa ni zawadi za viatu pea tano na soksi pea sita, kama sehemu
ya kuhamasisha uzingatiaji wa masomo na kuwajali watoto katika jamii.
Huu ni mfano bora wa juhudi za polisi katika
kuimarisha ulinzi na ustawi wa watoto, huku wito ukitolewa kwa kila mzazi
kushiriki kikamilifu katika kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Polisi wa Kata ya Kambarage, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi (A/INSP) Happiness Mathias Madondola, akizungumza na wazazi, walezi na wanafunzi wa shule ya msingi Kambarage kuhusu njia bora ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.