RAIS SAMIA ATOA ZAWADI ZA MWAKA MPYA KWA WATOTO YATIMA MIRERANI

 











Na Mwandishi wetu, Mirerani

RAIS Dkt Samia Suluhu Hassan ametoa zawadi za kumaliza mwaka 2024 na kuingia mwaka mpya wa 2025 kwa watoto yatima na wenye uhitaji maalum wa kituo cha Light In Africa kilichopo mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.

Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Fakii Raphael Lulandala imekabidhi zawadi hizo kwenye kituo hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Cuthbert Sendiga.

Kaimu Katibu Tawala wa Wilaya (DAS) Simanjiro, Tumaini Sebastian akiongozana na Ofisa mtendaji mkuu wa mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani (TEO) Isack Mgaya, ameyasema hayo wakati wa kukabidhi zawadi hizo kwenye kituo cha Light In Africa.

Tumaini amesema zawadi hizo zilizotolewa na Rais Dkt Samia kwenye kituo hicho ni mchele kilo 100, sukari kilo 25, unga ngano kilo 25, mafuta ya kupikia lita 20 na mbuzi wawili.

“Tunamshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwajali watoto yatima na wenye uhitaji maalum wa kituo hiki kilichopo mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kwa kuwapatia zawadi hizo za sikukuu,” amesema Tumaini.

Ametoa wito kwa watu binafsi, mashirika na taasisi mbalimbali kuwajali wenye uhitaji maalum na kushiriki pamoja nao kwa kuwapatia vyakula na vitu mbalimbali vya kujikimu.

Mmoja kati ya wasaidizi wa kituo hicho Mariam Mbwambo akizingumza wakati wa makabidhiano hayo, amemshukuru Rais Dkt Samia kwa kuwajali watoto hao na kutoa zawadi hizo kwao.

“Tunashukuru sana kwa zawadi hizi tunamuombea kwa Mungu ampe afya njema na uzima tele mama yetu na Rais wetu mpendwa Dkt Samia Suluhu Hassan,” amesema Mbwambo.
Previous Post Next Post