📌Mitungi ya gesi ya kupikia 3,255 kusambazwa Wilayani Uyui, Tabora.
📍Uyui
Mkuu wa wilaya ya Uyui, Mhe. Mohammed Mtulyakwaku amewataka Watanzania kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kuchochea ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 04, 2024 na Mhe. Mtulyakwaku mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa wilaya ya Uyui iliyowasilishwa na Mhandisi Ramadhani Mganga.
Amesema, Rais Samia amekuja na kampeni hii ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa na lengo la kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira ili kuboresha maisha ya wananchi.
Mhe. ameongeza kuwa, suala la Nishati Safi ya Kupikia sasa ni ajenda ya kimkakati na inayotakiwa kupewa kipaumbele na wataibeba katika kuelimisha umma kuhusu matumizi salama ya nishati hiyo kwa upana.
Kwa upande wake, Mha. Mganga amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kwamba hatua hiyo itawezekana kwa kupatikana kwa nishati safi ya kupikia iliyo nafuu na itumikayo kwa urahisi.
Ameongeza kuwa, mtoa huduma kampuni ya Taifa Gas Limited atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Tabora kwa kusambaza mitungi ya kilo sita 22,785 kwa bei ya ruzuku pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji na katika kila wilaya mitungi 3,255 itasambazwa.
Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Urambo, Uyui, Nzega, Sikonge, Kaliua, Igunga Na Tabora .