📌Mitungi ya gesi zaidi ya 22,785 kusambazwa mkoani Tabora
📌Kila wilaya kupatiwa mitungi ya gesi 3,255
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeingia mkataba na mtoa huduma kampuni ya Oryx Gas Tanzania Limited ambaye atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Tabora kwa kuuza kwa bei ya ruzuku mitungi ya gesi ya kilo sita pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji.
Hayo yamebainishwa leo Desemba 4, 2024 mkoani Tabora na Mhandisi wa miradi wa REA, Ramadhani Mganga wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ugawaji mitungi ya gesi ya kilo sita.
Mha. Mganga amesema kuwa mitungi ya gesi 22,785 itakayosambazwa mkoani Tabora itachochea kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati safi na salama.
"Lengo la mradi ni kukuza, kuchochea, kuwezesha na kuboresha upatikanaji wa huduma za nishati safi ya kupikia ili kupunguza ukataji wa miti ambapo takribani hekta 400,000 hukatwa kila mwaka, " Amesisitiza Mha. Mganga.
Mha. Mganga amesema, Serikali kupitia REA imetenga fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi (LPG) katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa mji na katika mkoa huo kiasi cha shilingi milioni 455.7 kimetengwa kutekeleza mradi huo.
Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Urambo, Uyui, Nzega, Sikonge, Kaliua, Igunga Na Tabora.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Wa Mkoa wa Tabora , Bw. Amos Ackim ameipongeza REA kwa kuja na mradi huo na kuiomba iwe endelevu ili iweze kuwasambazia wananchi wengi nishati hiyo muhimu Na kuchochea ustawi wa maisha ya wananchi.