Na Mapuli Kitina Misalaba
Serikali mkoani Shinyanga imetangaza kuzitumia timu
za Salawe FC na Solwa, zilizojipatia umaarufu kupitia Ligi ya Makamba Lameck,
kama sehemu ya burudani kwenye maadhimisho ya miaka 63 ya Uhuru wa Tanzania
Bara yanayofanyika kesho Desemba 9, 2024, katika uwanja wa Mhangu, Kata ya
Salawe.
Mbali na timu
za wanaume, mpira wa miguu kwa wasichana wa sekondari za Salawe na Mhangu pia
utakuwa sehemu ya burudani, ambapo wataonyesha vipaji vyao
kupitia mechi hiyo ya kirafiki
ikiwa ni juhudi za serikali kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye michezo.
Hatua hiyo imekuja baada ya timu hizo kuvutia
mashabiki wengi kwenye mashindano ya Makamba Lameck na kuonyesha mchango mkubwa
wa ligi hiyo katika kukuza vipaji vya vijana.
Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha ambapo wakazi wa Shinyanga na
vitongoji vyake wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kusherehekea siku hiyo muhimu
ya kihistoria.