Na Mapuli Kitina Misalaba
Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga
imefanya kitendo cha huruma kwa kutoa msaada kwa walemavu na wazee wanaoishi
katika kambi ya walemavu ya Busanda Misheni, ikiwa ni sehemu ya kusherehekea
Mwaka Mpya 2025 kwa furaha.
Kambi hiyo inahifadhi familia 14 zenye changamoto
mbalimbali, ikiwemo walemavu wa viungo, wazee wenye ukoma na wakongwe.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Bi. Husna Ally,
akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo, amesema kuwa msaada huo umetokana
na kuguswa na hali ya watu wa kambi hiyo.
"Sisi
Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga tumeweza kuguswa na hii kambi ya kulelea
walemavu wenye ukoma. Tukaona tujichange kidogo tulichobarikiwa na Mungu
tuwaletee ili waweze kusherehekea Mwaka Mpya kwa furaha,"
amesema Bi. Husna.
Msaada uliotolewa unajumuisha: Mfuko mmoja wa sabuni,
Mchele kilo 50, Ndoo ya sabuni, Maharage, Juice, Biskuti pamoja na Nguo
mbalimbali.
Bi. Husna pia ametoa wito kwa jamii kutoonyesha
unyanyapaa kwa watu wanaoishi katika kambi hiyo na kuwashauri watu kujitolea
kila inapowezekana.
Makamu Mwenyekiti wa Taasisi hiyo, Bi. Esther Shida,
amesisitiza kuwa msaada huo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Samia
Suluhu Hassan.
"Hizi
ni kazi ambazo tunamuunga mwanamke mwenzetu ambaye ni jemedari wa Tanzania,
Mama Samia. Tunaendelea kuwajibika kama yeye anavyowajibika. Hizi kazi ni
mwendelezo; tumekuwa tukisaidia sehemu mbalimbali kwenye Mkoa wetu huu wa
Shinyanga," amesema Esther.
Aidha, Bi. Esther ametaja changamoto ya maji safi
kama moja ya matatizo makubwa yanayowakabili wakazi wa kambi hiyo ambapo ametoa
wito kwa wadau wengine kuungana nao ili kuhakikisha wazee na walemavu hao
wanapata maji safi na salama kwa matumizi yao.
Katibu wa Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa
Shinyanga Bi. Tatu Juma Almas, ameeleza kuwa tukio hilo linaendana na maono ya
serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
"Leo
Desemba 31, 2024, Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga tumekuja hapa kwenye
kambi ya watu wenye ulemavu iliyopo Parokia ya Busanda. Tumeleta zawadi kwa
ajili ya sikukuu ya Mwaka Mpya kwa walemavu na wazee wa kambi hii. Hii yote ni
katika kuunga mkono kazi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya
mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan," amesema Tatu.
Msimamizi wa kambi hiyo, Kateksta Martin Sheka, ametoa
shukrani za dhati kwa msaada huo, akisema kwamba msaada huo utaleta furaha
kubwa kwa wakazi wa kambi hiyo.
"Ninawashukuru
sana Wanawake na Samia kwa hiki ambacho mmekileta katika kambi hii ya walemavu.
Msaada huu tunaupokea kwa shukrani kubwa na Mungu azidi kuwabariki zaidi maana
mmetufanya nasi tuweze kufurahia sikukuu ya Mwaka Mpya,"
amesema Seka.
Sheka pia ameeleza matumaini ya kambi hiyo kupokea
msaada zaidi kutoka kwa wadau kwa changamoto ya maji safi, huku akitoa salamu
za shukrani kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuwajali wanawake
na kuwapa nafasi zaidi za kiuchumi.
Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga wakiwasili
katika kambi hiyo ya walemavu Busanda Misheni leo Desemba 31, 2024.
Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa Shinyanga wakiwasili
katika kambi hiyo ya walemavu Busanda Misheni leo Desemba 31, 2024.
Katibu wa Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa
Shinyanga Bi. Tatu Juma Almas akizungumza wakati wa kukabidhi msaada kwenye
kambi ya walemavu Busanda Misheni leo Desemba 31, 2024.
Katibu wa Taasisi ya Wanawake na Samia Mkoa wa
Shinyanga Bi. Tatu Juma Almas akizungumza wakati wa kukabidhi msaada kwenye
kambi ya walemavu Busanda Misheni leo Desemba 31, 2024.