Na Mapuli Kitina Misalaba
Uwanja wa ndege wa Mkoa wa Shinyanga umefikia
takribani asilimia 80 ya utekelezaji wake, ukiwa ni sehemu ya juhudi za
serikali kuboresha miundombinu ya usafiri nchini na kwamba Mradi huo wa
kimkakati unatarajiwa kukamilika ifikapo Aprili Mwaka 2025.
Hayo yamezungumzwa na Mwakilishi wa wakala wa serikali wa usimamizi
wa barabara kuu na barabara za mikoa nchini Tanzania (TANROADS) Mkoa wa
Shinyanga Mhandisi Chiyando Matoke, Waandishi wa habari kutoka Mkoa wa
Shinyanga kupitia Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (Shinyanga
Press Club - SPC), kufanya ziara katika eneo la mradi ili kushuhudia maendeleo
ya ujenzi huo.
Matoke amesema ujenzi wa kiwanja hicho ulianza
Aprili 2023 na unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 49.18, ukiwa umefikia
hatua kubwa, ikiwemo kukamilika kwa barabara ya ndege (runway) yenye urefu wa
kilomita 2.2 ambapo amesema kazi zinazobaki ni pamoja na ujenzi wa jengo la
abiria na uzio wa kiwanja hicho.
"Nichukue nafasi hii kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa anazozifanya katika
kuboresha miundombinu ya nchi, ikiwemo viwanja vya ndege."
"Eneo la uwanja wa ndege kwa ajili ya kuruka na kutua ndege
limekamilika na linaweza kutumika. Uwanja huu una urefu wa kilomita 2.2, huku
kila mwisho wa barabara ya ndege kukiwa na kipande cha mita 300 cha hifadhi ya
urefu."
"Kwa sasa tunaendelea na ujenzi wa uzio wa uwanja huu, pamoja na
kipande cha barabara kinachounganisha barabara kuu na eneo la uwanja wa ndege
katika kiwango cha Lam"
"Tunaahidi serikali kwamba, kama tulivyoeleza kwa Naibu Waziri,
tutafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha uwanja huu unakamilika kwa
wakati." amesema Matoke.
Kwa upande wake, Mhandisi Ruburi Kahatano wa Kampuni
ya CHICO, ambayo inatekeleza mradi huo, amesema ndege mbili za dharura
zimeshatua katika kiwanja hicho, ikiwemo moja iliyombeba mgonjwa kwenda Dar es
Salaam kwa matibabu ya dharura.
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa
Shinyanga, Greyson Kakuru, amepongeza serikali kwa juhudi zake za kuboresha
miundombinu, akisema kukamilika kwa kiwanja hicho kutaleta fursa za kiuchumi
kwa wakazi wa Shinyanga na maeneo jirani.
Viongozi mbalimbali wanahusika na
ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga wakiwaongoza waandishi wa habari
kutembelea kiwanja cha ndege leo Desemba 23, 2024.
Viongozi mbalimbali wanahusika na
ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga wakiwaongoza waandishi wa habari
kutembelea kiwanja cha ndege leo Desemba 23, 2024.
Viongozi mbalimbali wanahusika na
ujenzi wa Kiwanja cha Ndege Shinyanga wakiwaongoza waandishi wa habari
kutembelea kiwanja cha ndege leo Desemba 23, 2024.