Na Lucas Raphael,Tabora
Serikali imetoa vifaa mbalimbali kwa halmashauri ya Wilaya ya Nzega mkoani Tabora kwa ajili ya wanafunzi wenye Mahitaji Maalum, vimetoletwa kwa ajili ya wanafunzi wa shule za Msingi na Sekondari vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 30.
Akikabidhi vifaa hivyo mkurungezi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega, mhandisi Modest Apolinary alisema kwamba serikali kupitia ofisi ya Rais Tanmisemi imetoa vifaa hivyo ili kuweza kuwasaidia watoto wenye uhitaji .
Alisema kwamba vifaa hivyo vimetolewa kwa watoto wenye Ulemavu wa Viungo ambao wamepatiwa vitimwendo 11 , magongo 17 na walemavu wa ngozi wamepatiwa kofia na mafuta ya kupaka yaani (Lotion).
Alitaja vingine ni Vifaa kwa ajili ya wanafunzi viziwi na Vifaa kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili.
Alisema vifaa hivyo vitumike kwa malengo yaliyokusudiwa kwa ajili ya kuwarahisishia huduma watoto wao na kuunga mkono juhudi za wazazi na walezi wa watoto wenye uhitaji .
Awali afisa elimu, elimu maalum msingi wa halmashauri ya Wilaya ya Nzega Joshua Samson alisema kwamba Divisioni ya elimu msingi ilifanya utambuzi wa watoto wote wenye kustahili kupewa vifaa hivyo.
Alisema kwamba vifaa vyote vitagawanywa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na vifaa vingine vitagawanywa kwenye vitengo vya elimu maalum katika shule za Iyombo,Isimba na Mahene.
Alisema kwamba kutolewa kwa vifaa hivyo kutasaidia sana wanafunzi wa elimu ya awali na wale wa msingi na sekondari kwani wengi walikuwa na changamoto kufika haraka shuleni .
Naye Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwambaha Daud Mwakanusya aliipongeza serikali kwa kutoa vifaa hivyo kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum ambavyo nitawasaidia kufika haraka shule na mahudhurio yao yataongezeka tofauti na hapo awali .
Mkurungezi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nzega, mhandi ModestApolinary Alipokuwa wakiwapatia (Lotion) watoto wenye ulemavu wa ngozi .