Watanzania wametakiwa kutoona kero kuhusu madai ya Katiba mpya, kwa kuwa suala hilo lina lenga kuondoa hali ya kundi dogo kuwaonea wengine kupitia nguvu linayoipata katika katiba ya sasa.
Kibamba amebainisha kuwa, Katiba ya sasa pamoja na kufanyiwa marekebisho mara 14 kabla na baada ya uhuru, bado haikidhi mahitaji yanayozingatia maslahi ya wananchi, kwa kuwa haitokani na maoni yao, na badala yake inawapendelea zaidi watawala.
Amesema Katiba hiyo ilianza kwa kuandikwa na kupitishwa na Bunge la Uingereza mara tu baada ya Tanganyika kupata uhuru, lakini iliendelea kufanyiwa marekebisho ili kutosheleza mahitaji ya kisiasa bila kushirikisha wananchi kwa kuondoa ama kuongeza vifungu kadhaa, hatua ambayo inaifanya kuwa na kasoro nyingi zinazowanyima wananchi nguvu ya kujitawala kulingana na jinsi ambavyo wanaona inafaa.
Kibamba amewataka watanzania kutopuuza au kuona kero juu ya madai ya Katiba mpya na kwamba, changamoto za kiuchumi, kisiasa na kijamii wanazokutana nazo zinatokana kwa kiasi kikubwa na katiba iliyopo kuwaweba watawala zaidi badala ya wananchi, hatua ambayo inasababisha kundi fulani la watu kulionea kundi jingine.
Amewataka wananchi kutambua kuwa, suala la katiba mpya siyo la kuwaachia wanasiasa pekee bila wao kuwa mstari wa mbele kuidai kwa njia zinazofaa bila kuhatarisha hali ya amani, kwa kuwa wanasiasa wanaangalia zaidi maslahi yao ya kisiasa jambo ambalo lilikwamisha kupitishwa kwa rasimu ya Katiba ya Jaji Mstaafu Joseph Sinde Warioba, baada ya Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuonesha nia njema ya kuanzisha mchakato wa Katiba mpya inayotokana na maoni ya wanachi.
Kwa upande wake Mwanaharakati wa haki za binadamu na masuala ya jinsia Dkt. Ananilea Nkya, alibanisha kuwa, ili Katiba iwe bora na inayofaa, lazima iwe imetokana na maoni ya wananchi ili wao wenyewe waeleze ni kwa namna gani wanataka kujiendesha kiuchumi, kisiasa na kijamii, badala ya kuandaliwa na kikundi cha watu wachache wanaojali maslahi yao binafsi.
Dkt.Nkya ameendelea kufafanua kuwa, endapo Katiba mpya itapatikana itasaidia kudhibiti hali ya viongozi wachache kutumia madaraka yao kujinufaisha na raslimali za taifa.
Amewataka watanzania kusimama nafasi ya mbele kupigania Katiba mpya ikiwemo tume huru ya uchaguzi ambayo itakuwa haina mgongano wa kimaslahi na watawala, ili chaguzi ziwe huru na za haki na kuwawezesha kuwapata wawakilishi wanaowataka, badala ya kuwaachia jambo hilo wanasiasa pekee, hatua ambayo imekuwa ikisasabaisha migogoro mingi na kuhatarisha amani wakati na baada ya uchaguzi.
Naye Mwanasheria wa JUKATA Bw. Thobias Messanga alitumia kongamano hilo la Katiba kuwataka wananchi kuunga mkono juhudi za madai ya Katiba mpya ili kuwa na Demokrasia ya kweli na kwamba, bila watu kuungana kwa pamoja haiwezi kupatikana.
Kwa upande wao wananchi waliohudhuria Kongamano hilo lililofanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Karena mjini Shinyanga, walieleza shauku waliyonayo katika kupata Katiba mpya huku wakikiri kwamba, inayotumika hivi sasa ina mapungufu mengi ikiwemo kuwanyima fursa ya kuwapata wawakilishi wanaowataka katika vyombo vya maamuzi.
Wananchi hao pamoja na kutaka suala la amani kupewa kipaumbele katika mchakato wa madai ya Katiba, wameomba elimu iendelee kutolewa zaidi ili watanzania wote watambue umuhimu wa Katiba mpya, badala ya ilivyo hivi sasa ambapo baadhi yao wamekuwa wakiungana na wanasiasa wasio na nia njema kuhoji endapo katiba mpya inaweza kuleta maendeleo.