Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa jamii kuacha mila za ukeketaji badala yake kuwapa watoto wa kike maisha yenye heshima, usalama, na ustawi wa afya.
Dkt. Gwajima amezungumza hayo katika kilele cha maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia kilichofanyika mkoani Mara.
“Ukeketaji kwa kisingizio cha mila na desturi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazowaathiri watoto wa kike na wanawake nchini. Ingawa utafiti wa Kitaifa wa Idadi ya Watu na Afya Tanzania (TDHS-2022) unaonesha kupungua kwa asilimia 2 ya ukeketaji ila baadhi ya maeneo bado yanaonesha ongezeko la vitendo hivyo” amesema Dkt.Gwajima.
Dkt. Gwajima ametoa wito kwa viongozi wa dini na kimila kuhamasisha mila chanya na kupinga ukatili wa kijinsia, kwa kuelimisha jamii, na kuvitaka vyombo vya habari na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuendeleza juhudi za kuhamasisha jamii na kusaidia waathirika.
“Tunapojadili masuala ya ukatili wa kijinsia, ukeketaji ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazowakumba watoto wa kike, wasichana, na wanawake. Ingawa tumepiga hatua katika kupunguza vitendo hivi ila bado kiwango cha ukeketaji ni cha juu zaidi vijijini kuliko mijini, niwaombe viongozi wa dini na kimila Kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi Kwa pamoja tuungane kutoa elimu ya kupinga vitendo hivi kwani ni ukatili mkubwa dhidi ya mtoto wa kike” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya, ameeleza kuwa juhudi za kutoa elimu kwa jamii zimesaidia kupunguza vitendo vya ukatili wa kijinsia na hivyo kuushusha mkoa wa Mara kutoka nafasi ya kwanza hadi ya tatu kwa matukio ya ukatili nchini.
Aidha, Mratibu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPFNet), Naibu Kamishana wa Polisi (DCP) Maria J. Nzuki, amesisitiza kuwa Maadhimisho ya siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia siyo mwisho wa juhudi hizo, na kwamba Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na wananchi kwa kutoa elimu na kuchukua hatua thabiti za kudhibiti na kutokomeza ukatili wa kijinsia, ikiwa ni pamoja na mila kandamizi kama ukeketaji katika mkoa wa Mara na Mikoa mingine.