ZAIDI YA WATOTO 36,000 WANAISHI MITAANI KAHAMA, WATOTO WATOA KILIO CHA UKATILI

Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imeadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, ambapo changamoto kubwa imeibuliwa kuhusu maisha ya watoto wanaoishi mitaani.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Robert Kwela, amesema zaidi ya watoto 36,000 wanaishi mitaani katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

Amesema ukosefu wa makazi maalum kwa watoto hao unachangia kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi yao.

Afisa Uhamiaji wa Wilaya ya Kahama, Salum Rashid, ameongeza kuwa kiwango cha utumikishwaji wa watoto, hasa kutoka mataifa jirani, kimeongezeka ambapo kazi za nyumbani zimeonekana kuwa eneo linaloathiriwa zaidi, huku wanawake wakitajwa kuongoza katika kuajiri watoto kwa njia zisizo halali.

Wakati huo huo, baadhi ya watoto waliohudhuria maadhimisho hayo wameiomba serikali kuweka juhudi zaidi katika kupambana na ukatili wa kijinsia.

Wameeleza kuwa vitendo hivyo haviharibu tu maisha yao ya sasa bali pia vinaathiri maendeleo yao ya kitaaluma.

Maadhimisho hayo ni sehemu ya jitihada za kuhamasisha jamii kupinga ukatili wa kijinsia na kulinda haki za watoto katika mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine nchini.

TAZAMA VIDEO

Previous Post Next Post