ZAIDI ya shilingi milioni 400 zimekusanywa katika Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Ziwa Duluti ikiwa ni mapato yaliyotokana na wageni wa ndani na nje kwenda kutalii katika Ziwa hilo lililopo Mkoani Arusha.
Hayo yalisemwa na Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania{TFS} Ziwa Duluti,Peter Myonga mara baada ya wahasibu kutoka nchi mbalimbali Afrika kutembelea Ziwa Duluti.
Alisema mapato ya serikali katika Msitu wa Ziwa Duluti yamekuwa yakipanda mwaka hadi mwaka kutokana na watalii wengi wa ndani na nje kwenda kutalii katika Ziwa Duluti na kujionea vivutio mbalimbali adimu vilivyoko katika Msitu huo.
Myonga alisema mwaka mwaka wa fedha julai 2022/23 watalii wa ndani 16,760 walitembelea Ziwa Duluti ikiwa ni pamoja na watalii wa nje 6,700 na shilingi milioni 46 zilikusanywa kama mapato ya serikali.
Alisema katika kipindi cha mwaka 2023/24 jumla ya shilingi milioni 106 zilikusanywa ikiwa ni mapato ya wageni kutoka ndani ya nchi na nje na kuvuka malengo ya mwaka uliopita.
Mhifadhi huyo Mkuu alisema kuwa katika muda mfupi wa miezi mitano cha kuanzia julai 2024/25 hadi novemba mwaka huu watalii wa ndani waliokwenda kutembelea Ziwa Duluti ni watalii 8,680 na wageni kutoka nje ya nchi watalii 7000 na mapato ya serikali milioni 70 yamekusanywa hiyo ni miezi minne tu kiasi hicho kimekusanywa na huenda hadi kufika june mwakani makusanyo yanaweza kuvuka malengo zaidi.
Myonga alisema kuwa Utalii uliopo katika Msitu wa Hifadhi ya Ziwa Duluti ni pamoja na utalii wa Majini,Utalii wa Msitu,Utalii wa Uvuvi wa Samaki,Utalii wa Picha,Utalii wa Utafiti,Utalii wa kutembea bila viatu{pekupeku} na Utalii wa maombi.
Alisema watalii wengi wa ndani wanakwenda kutalii katika Msitu wa Ziwa Duluti kwa ajili ya utalii Utalii wa Maombi hususani siku za wiki za mapumziko kazi kwani mamia ya watanzania huenda katika Hifadhi hiyo kutalii Utalii wa Maombi na kuingizia serikali mapato.
Mhifadhi Mkuu Myonga alisema mbali ya Utalii wa Maombi na vivutio vingine ambavyo kwa pamoja vimewapa ajira vijana zaidi ya 200 kwa kununuwa mitumbwi na kutembezwa katika ziwa Duluti na kuwa na uhakika wa kipato kwa siku.
‘’Kwa sasa Hifadhi ya Msitu wa Asili wa Ziwa Duluti imekuwa chanzo kikubwa cha mapato Mkoani Arusha hivyo serikali imeweka nguvu kubwa katika Hifadhi hiyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha inavutia wawekezaji kuwekeza katika ziwa hilo’’alisema Myonga
Naye Afisa Utalii wa Wakala wa Misitu na huduma Tanzania{TFS} katika Hifadhi ya Ziwa Duluti ,Anna Lawuo alisema shughuli za uvunaji hazifanyiki katika Msitu wa Hifadhi ya Ziwa Duluti kwani utalii wa Ikolojia tu ndio unaofanyika na kuingiza serikali mapato.
Lawuo alisema Msitu huo una ndege ambao hawako katika Hifadhi nyingine na ni kivutio kikubwa kwa watalii wa ndani na nje na kuna utulivu mkubwa ambao huwavutia watalii wengi kwenda kutalii .
Naye Mtalii aliyekwenda kutalii katika Ziwa Duluti aliyejitambulisha kwa jina la Abas Mohamed kutoka Kenya alisema kuwa amevutiwa na hali ya asili iliyokuwa katika msitu huo na kuonyesha wazi kuwa Tanzania ina vitu vingi vya kuingizia nchi mapato na vikitangazwa kikamilifu nchi itakuwa na mapato ya kutosha.