Baba Mtakatifu Fransisko, amemteua Padre Romanus Elamu Mihali, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Iringa, baada ya kuridhia ombi la kustaafu kwa mujibu wa sheria za Kanisa kwa aliyekuwa Askofu wa Jimbo hilo Mhashamu Tarcisius Ngalalekumtwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC, Padre Chesco Msaga, Padre Mihali ameteuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Iringa Jumanne tarehe 28.01.2025.
Askofu Mteule Romanus Mihali alizaliwa mnamo Juni 10 mwaka 1969 katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa.
Baada ya kumaliza masomo yake ya kipadre, alipewa Daraja takatifu la Upadre mnamo Julai 13 mwaka 2000, ambapo alihudumu katika nafasi mbalimbali Jimboni Iringa.
Alijiendeleza kielimu katika chuo kikuu cha Kerala nchini India na kutunikiwa shahada ya Uzamili katika Sayansi ya wanyama mwaka 2010.
Mpaka kuteuliwa kwake, alikuwa Makamu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mafinga.
Aidha kufuatia Askofu Ngalalekumtwa kukubaliwa ombi lake la kustaafu, kwa sasa ataendelea kuwa msimamizi wa kitume wa Jimbo la Iringa mpaka Askofu mteule Mihali atakapowekwa wakfu na kusimikwa kuliongoza Jimbo hilo.
Waamini wa Jimbo Katoliki Shinyanga wakiongozwa na Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, wanamtakia matashi mema na kumwombea kwa Mungu ili ampe nguvu na neema Askofu mteule Mihali pale anapojiandaa kupokea jukumu alilopewa na Kanisa la kuliongoza Jimbo la Iringa.