Na Mapuli Kitina Misalaba
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jimbo la
Shinyanga Mjini, Viongozi na wanachama wa chama hicho wameazimia kumuunga mkono
Tundu Lissu katika kinyang’anyiro cha nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa
kwenye uchaguzi unatarajiwa kufanyika
Januari 21, 2025.
Wameyasema hayo wakati wakizungumza na Misalaba
Media baada ya kufanya maazimio yao kwenye kikao cha mkutano mkuu maalum wa
jimbo hilo.
Mkutano huo, umefanyika kwa lengo la kujadili
masuala mbalimbali ya chama, ambao umehudhuriwa na viongozi wakuu wa jimbo hilo, wakiwemo
Mwenyekiti wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini, Bwana Hamis Ngunila, Katibu wa
Jimbo, Bwana Sebastian Polepole, pamoja na wajumbe na wanachama kutoka matawi
na kata mbalimbali.
Katika mjadala kuhusu uchaguzi wa Mwenyekiti wa
CHADEMA Taifa, wanachama wameonyesha kumuunga mkono Tundu Lissu, ambaye kwa
sasa ni Makamu Mwenyekiti wa chama ambapo wamesema kuwa wanamuona kama kiongozi
mwenye uwezo wa kuleta mabadiliko na matumaini mapya ndani ya chama.
Baadhi ya wanachama wametoa maoni yao wakisema kuwa
Freeman Mbowe, ambaye ameshikilia nafasi ya Mwenyekiti kwa miaka 21, anapaswa
kupumzika na kuwa mshauri wa chama.
“Muda
umefika wa kumpumzisha Freeman Mbowe. Tumekuwa tukipitia changamoto nyingi,
ikiwemo uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 ambapo tuliona majina ya
wagombea wetu yakikatwa na kura bandia zikichukuliwa. hadi sasa, hatujamuona
akikemea suala hilo kwa ukali. Ni wakati wa Lissu kuleta mabadiliko,” .
Wanachama wengine wamesisitiza kuwa Tundu Lissu
ndiye kiongozi anayefaa kusimamia chama wakati huu.
“Maisha
ambayo tumeyapitia yanatosha. Tarehe 21 hatutakosea, Tundu Lissu ndiye
Mwenyekiti atakayepeperusha bendera ya CHADEMA Taifa,” .
“Tunamtaka Tundu Lissu kwa sababu ndiye tiba
ya CCM. Mbowe tayari CCM walishamzoea, wanajua jinsi ya kushirikiana naye CCM
wanafanya uchaguzi wanavyotaka,”.
Wanachama wa CHADEMA Jimbo la Shinyanga Mjini
wamesema kuwa wao kwa pamoja wameamua kumuunga mkono Tundu Lissu na wametoa
wito kwa wanachama wengine wa CHADEMA nchini kufanya hivyo.
“Jimbo
la Shinyanga Mjini tuko pamoja na Tundu Lissu. Tunaamini ana uwezo wa kuleta
matumaini na mwelekeo mpya kwa chama chetu,”.
Aidha, wamesisitiza kuwa uchaguzi wa Januari 21,
2025, ni fursa ya kuimarisha chama kwa kumchagua kiongozi mpya mwenye maono na
nguvu ya kuendeleza harakati za kisiasa nchini.
“Tunatoa wito kwa wanachama wote wa CHADEMA
nchini kuchagua kiongozi ambaye ataipeleka mbele agenda ya mabadiliko. Tuna
imani kuwa Tundu Lissu ndiye mtu sahihi kwa nafasi hiyo,”.
Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA
unatarajiwa kuwa wa kihistoria, huku wanachama wengi wakiwa na matumaini
makubwa ya kuona mabadiliko makubwa ndani ya chama.