MZEE MMOJA AFARIKI KWA KUJINYONGA MANISPAA YA SHINYANGA FAMILIA YATOA SIMULIZI WATU WANNE WA FAMILIA MOJA KUFARIKI KWA KUJINYONGA MMOJA KUOKOLEWA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mzee Joseph Shija mwenye umri wa Miaka 75, mkazi wa mtaa wa Azimio katika kata ya Lubaga, Manispaa ya Shinyanga, amefariki dunia kwa kujinyonga ndani ya nyumba yake.

Tukio hilo limetokea Januari 6, 2025 ambapo taarifa za kifo cha mzee huyo zimethibitishwa na diwani wa kata ya Chibe, Mhe. Kisandu John, ambaye pia ni baba mdogo wa marehemu ambaye amezungumza kwa niaba ya familia, akieleza jinsi alivyopokea taarifa za tukio hilo.

“Mimi nilipewa taarifa hii jana saa kumi jioni kutoka kwa majirani waliona nzi wengi kwenye dirisha la nyumba yake, jambo ambalo liliwashangaza na kuwafanya waanze kutupigia simu sisi ndugu,” amesema Mhe. Kisandu.

Aliongeza kuwa baada ya kufika eneo la tukio, alitoa taarifa kwa polisi ambao walivunja mlango wa nyumba hiyo na kukuta mwili wa mzee Shija akiwa amejinyonga kwa kutumia kamba aliyofunika na shuka lake.

Kwa mujibu wa maelezo ya familia, marehemu alikuwa akiishi peke yake baada ya mkewe kuwa mgonjwa kwa takribani miaka minne ambapo watoto wake wanafamiliazao mbali na nyumbani na kwamba historia ya familia hiyo, marehemu Joseph Shija anakuwa mtu wa nne kufariki kwa kujinyonga.

“Hatujui sababu iliyopelekea mzee huyu kufikia hatua ya kujinyonga, lakini historia ya familia ni ya kusikitisha. Yeye anakuwa mtu wa nne katika familia hii kufariki kwa kujinyonga alianza Mama yao, akaja kijana mmoja kutoka Kahama naye akajinyonga, na binti mwingine wa familia hiyo wote walijinyonga bila kutoa sababu, huku mwingine akinusurika baada ya kuokolewa,” amesema Mhe. Kisandu kwa huzuni.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo.

“Ni kweli, jana majira ya saa kumi na mbili jioni tulipokea taarifa za kifo cha Mzee Joseph Shija, ambaye alijinyonga kwa kutumia shuka alilofunga kwenye paa la nyumba yake, Uchunguzi wa awali unaonyesha chanzo kuwa ni msongo wa mawazo kutokana na maradhi yaliyokuwa yakimsumbua kwa muda mrefu,” amesema SACP Magomi.

Kamanda Magomi amesema mwili wa marehemu ulichukuliwa kwa uchunguzi wa kitabibu na tayari umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.
Kamanda Magomi ametoa wito kwa jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi, akisisitiza kuwa kujinyonga si suluhisho la changamoto za maisha.

“Kujichukulia sheria mkononi ni kosa vilevile kwa mtu wa umri wa miaka 75 kujinyonga haionyeshi mfano mzuri kwa jamii hasa watoto. Ni muhimu kwa wazazi, walezi, na jamii kwa ujumla kumtegemea Mwenyezi Mungu na kushirikisha wengine pale tunapokumbwa na changamoto,” amesema.
Mazishi ya mzee Shija tayari yamefanyika leo katika mtaa wa Azimio kata ya Lubaga Manispaa ya Shinyanga.

 

Previous Post Next Post