POLISI WAMKAMATA MTUHUMIWA WA PICHA ZA UTUPU ZILIZOSAMBAZWA KINYUME NA SHERIA

Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia mtuhumiwa mmoja jina limehifadhiwa kwa tuhuma za kukutwa na picha mjongeo za utupu zenye maudhui machafu kimaadili kinyume na Sheria na kifaa cha kielektroniki ambacho alikuwa akitumia kusambaza picha hizo chafu.

Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Salim Moracase, akizungumza na vyombo mbalimbali vya habari baada ya kupokea taarifa kutoka kwa uongozi wa Shule ya Baobab, iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani amesema waliotengeneza picha waliunganisha na baadhi ya majengo ya shule ili kuaminisha umma kuwa vitendo hivyo vinafanyika shuleni hapo.

“Jeshi la polisi limefanya uchunguzi limefanikiwa kumkamata mtu mmoja ambaye uchunguzi wa kitaalamu ulisaidia kumfikia na kumkuta na picha hizo na kifaa ambacho alikuwa akitumia kusambaza picha hizo chafu," alisema Moracase.

Aidha, Kamanda Moracase amesema wanaendelea kuwasaka watu wengine waliohusika katika kutengenezea na kusambaza picha hizo.

Jeshi hilo limetoa onyo kwa watu wenye tabia kama hizo za kutengengeneza picha kama hizo kwa malengo ya kuchafua wengine au Taasisi kwani mkono wa sheria lazima utawafikia.

Previous Post Next Post