JUMUIYA YA WAZAZI CCM SHINYANGA YAAZIMISHA MIAKA 48 YA CCM KWA USAFI, UTOAJI DAMU SALAMA NA MSAADA KWA WAHITAJI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini leo Januari 29, 2025 imeadhimisha miaka 48 ya CCM kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii, ikiwemo usafi wa mazingira, uchangiaji wa damu salama katika Kituo cha Afya Ihapa, na kutoa msaada wa vitu mbalimbali kwa wahitaji.

Katika maadhimisho hayo, viongozi wa jumuiya hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti Fue Mrindoko, Katibu Bi. Doris Yotham Kibabi, na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Mary Makamba, wametembelea kata kadhaa kushiriki shughuli hizo.

Viongozi hao wamefika katika Soko la Wajasiriamali Ibinzamata, ambako wameshirikiana na wanachama wa kata hiyo kufanya usafi na kuzungumza na wajasiriamali wa soko hilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Fue Mrindoko, amewasisitiza wafanyabiashara hao kutunza miundombinu ya soko hilo huku akiipongeza serikali kwa kulijenga, jambo ambalo limewaondolea usumbufu na kuwaimarisha kiuchumi.

Baadhi ya wajasiriamali wametoa shukrani kwa jumuiya hiyo kwa kufanya usafi katika eneo hilo na kuwasikiliza changamoto zao ambapo Mrindoko amemhimiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga kushughulikia changamoto zilizopo sokoni hapo.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Bi. Doris Yotham Kibabi, amewapongeza viongozi wa matawi na wanachama kwa kushiriki katika usafi huo na akawataka kuendelea na juhudi hizo maeneo mengine kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 48 ya CCM huku akisisitiza kuwa utunzaji wa soko hilo ni jukumu la wajasiliamali wenyewe.

"Soko hili tumejengewa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini jukumu la kulitunza ni letu sote. Tusipolitunza, litaharibika mapema. Napenda kuipongeza serikali kwa kujenga soko hili la kisasa, kwani awali walikuwa wanafanya biashara chini ya maturubai," amesema Doris.

Baada ya shughuli za usafi sokoni, viongozi hao wameelekea katika Kituo cha Afya Ihapa kilichopo Kata ya Old Shinyanga, ambako wameshirikiana na viongozi wa jumuiya hiyo kufanya usafi wa mazingira na kuchangia damu salama.

Kwa niaba ya Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Daktari Joel Kapinga ameishukuru jumuiya hiyo kwa kushiriki katika zoezi la uchangiaji damu na kufanya usafi ambapo amesema kuwa damu iliyokusanywa itasaidia kuokoa maisha ya wagonjwa wenye uhitaji.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Fue Mrindoko, amewapongeza madaktari kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kituo cha Afya Ihapa na kwamba amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kuboresha sekta ya afya, elimu, na miundombinu.

"Tuna kila sababu ya kumpongeza Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kujenga shule, hospitali, barabara na madaraja makubwa na madogo kote nchini amefanya kazi nzuri sana," amesema Mrindoko.

Aidha, amezungumzia maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM wa Dodoma, ambapo Rais Samia alipitishwa kuwa mgombea pekee wa chama hicho kwa nafasi ya urais katika uchaguzi ujao ambapo amesema kuwa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini imekubali maamuzi hayo na wanaendelea kumuunga mkono.

Katika hotuba yake, Mrindoko ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwa makini katika malezi ya watoto wao na kuhakikisha kuwa wanawafundisha maadili mema.

Amesisitiza kuwa wale wanaofanya ukatili dhidi ya watoto, ikiwemo ubakaji na ulawiti, wanapaswa kuchukuliwa hatua kali za kisheria badala ya kumaliza kesi hizo kifamilia.

"Wazazi wanapaswa kuwa makini na watoto wao. Vijana wengi wanaharibika kutokana na kuchezewa na wahuni. Wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watoto wao hawapotei," amesema Mrindoko.

Kwa mujibu wa Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Yotham Kibabi, maadhimisho hay oleo yamefanyika katika kata mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Ndembezi, Ibinzamata, Old Shinyanga, Lubaga, Kitangili, Kizumbi, na Ibadakuli ambapo amesema kuwa kata hizo zimefanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile usafi kwenye shule na masoko.

Doris ameongeza kuwa maadhimisho ya miaka 48 ya CCM yatahitimishwa kwa sherehe kubwa inayotarajiwa kufanyika Januari 31, 2025, katika Kata ya Chibe, Wilaya ya Shinyanga Mjini ambapo amewaomba viongozi, wanachama, na wananchi kuhudhuria kwa wingi ili kusherehekea mafanikio ya chama hicho tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977.

Katika kipindi cha miaka 48, CCM imeendelea kuwa chama kinachoongoza nchi kwa sera na mikakati inayolenga kuleta maendeleo kwa wananchi wake, huku Jumuiya ya Wazazi ikiendelea kuwa mshirika muhimu katika kufanikisha malengo hayo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Fue Mrindoko, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Bi. Doris Yotham Kibabi na Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji jumuiya ya wazazi Bi. Mary Makamba wakishiriki na viongozi wa jumuiya hiyo kata ya Ibinzamata kufanya usafi wa mazingira katika eneo la soko la wajasiliamali Ibinzamata ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 48 ya CCM.




 

Previous Post Next Post