JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAHITIMISHA SHEREHE YA MIAKA 48 YA CCM KWA MATENDO, FUE MRINDOKO ATOA WITO KWA WANAFUNZI NA WAZAZI

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga mjini Fue Mrindoko, akizungumza kwenye hitimisho la maadhimisho ya Miaka 48 ya CCM ambapo jumuiya hiyo imehitimisha leo Januari 31, 2025 katika shule ya sekondari Mwangulumbi kata ya Chibe.


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga mjini Fue Mrindoko, amewataka wanafunzi kuzingatia elimu na kuepuka kurubuniwa katika vitendo vinavyoweza kuharibu maisha yao huku akisisitiza jukumu la wazazi kuwalea na kuwatunza watoto wao ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya uhalifu na maadili mabovu.

"Ninawaombeni sana wanafunzi mzingatie elimu, msirudi nyuma. Sisi wazazi ni jukumu letu kuwalea na kuwahudumia watoto hawa. Tusipowalea, watakuwa vibaka na kushiriki michezo michafu. Tukiwalea vizuri, tutawaepusha na ukatili. Wanafunzi, msimame imara na msikubali kuchezewa, maana maisha yenu yataharibika," amesema Mrindoko.

Mwenyekiti huyo amesisitiza umuhimu wa utunzaji wa mazingira, hasa katika shule, akiwataka wanafunzi na wazazi kuendelea kushiriki katika upandaji wa miti kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Mwenyekiti huyo amewahimiza wanajumuiya ya wazazi kuendelea kushirikiana ili kuimarisha jumuiya hiyo, hasa katika nyanja za afya, elimu na mazingira.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Yotham Kibabi, ameeleza shughuli mbalimbali zilizotekelezwa katika maadhimisho ya miaka 48 ya CCM.

"Tumeadhimisha sherehe hizi katika kata zote 17 kwa kufanya shughuli mbalimbali kama vile upandaji miti shuleni na vituo vya afya, utoaji wa vifaa vya elimu kwa wanafunzi, na kuchangia chakula mashuleni. Pia, tumefanikisha upimaji wa damu salama," amesema Bi. Doris.

Katika maadhimisho hayo, jumuiya hiyo imefanikiwa kupanda miche 891 ya miti, kugawa daftari zaidi ya 60, kalamu zaidi ya 50, kilo 225 za unga wa mahindi, mfuko wa sukari wa kilo 25, na debe sita za mahindi ambapo Shule zilizopokea msaada huo ni pamoja na Shule ya Msingi Msufini, Kitangili, Town, na Sekondari ya Mwasele.

Katika sherehe hizo, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mwangulumbi, iliyopo Kata ya Chibe Manispaa ya Shinyanga, wamebainisha changamoto wanazokabiliana nazo, ikiwemo uhaba wa matundu ya vyoo, ukosefu wa umeme, na ukosefu wa mabweni kwa wanafunzi wa kike.

Kaka mkuu na dada mkuu wa shule hiyo wamesema ukosefu wa umeme unatatiza masomo ya vitendo katika maabara, huku upungufu wa matundu ya vyoo ukisababisha msongamano mkubwa na kuhatarisha afya za wanafunzi.

Akijibu changamoto hizo, Diwani wa Kata ya Chibe, Kisandu John, ameeleza kuwa tayari shilingi milioni 44 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo, huku akiahidi kuwa suala la umeme litapewa kipaumbele ndani ya mwezi mmoja.

Shule ya Sekondari Mwangulumbi ina jumla ya wanafunzi 523 na inakabiliwa na upungufu wa matundu 15 ya vyoo.

Katika sherehe hizo, jumuiya hiyo imempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuleta maendeleo, ikiwemo ujenzi wa shule na hospitali na kwamba jumuiya hiyo imetangaza kuunga mkono maamuzi ya Mkutano Mkuu wa CCM ya kumpitisha Rais Samia kama mgombea wa urais kwa uchaguzi mkuu ujao.

"Tunaendelea kumuunga mkono Rais Samia na tunawahimiza wananchi wa Shinyanga kuhakikisha wanachagua madiwani, mbunge, na Rais kutoka CCM ili maendeleo yaendelee," amesema Bi. Doris.

Katika maadhimisho hayo, elimu kuhusu ukatili kwa wanafunzi na umuhimu wa uchangiaji damu salama pia imetolewa kwa washiriki.Viongozi wa jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini wakiwasili katika shule ya sekondari Mwangulumbi kata ya Chibe kwa ajili ya kusherehekea Miaka 48 ya CCM.


Previous Post Next Post