Na Mwandishi Wetu, Misalaba Media
Leo, jumuiya ya Wazazi kutoka CCM Kambarage imetembelea Shule ya Sekondari Mwasele kwa lengo la kuadhimisha maadhimisho ya wazazi, kuhamasisha utunzaji wa mazingira, na kuimarisha maendeleo ya wanafunzi shuleni. Ujio wa kamati hii umeleta mabadiliko makubwa kwa shule, ukitoa mafundisho yenye msukumo kwa wanafunzi, walimu, na wazazi kwa ujumla.
Mwanafunzi mmoja alieleza furaha yao kwa kutembelewa na kamati hiyo, akisema:
"Ujio wao umetupa mafunzo mbalimbali kuhusu nidhamu, utii, na jinsi ya kuepuka vitendo vya ukatili. Pia wametufundisha kupenda mazingira kwa kutuletea miti na kutusisitiza umuhimu wa chakula shuleni."
Kwa upande wa walimu, Mwalimu Leonard Mapolu aliwashukuru wageni kwa mchango wao wa thamani kwa shule hiyo, akisema:
"Kamati ya Wazazi CCM hawajaja mikono mitupu. Wamekuja na miti wakihamasisha utunzaji wa mazingira sambamba na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan. Pia wametuletea chakula kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanapata mlo shuleni, jambo linaloimarisha uwezo wao wa kujifunza kiakili na kisaikolojia. Tunatoa wito kwa wazazi wote kushirikiana kuhakikisha watoto wanapata chakula shuleni na kuunga mkono juhudi hizi za maendeleo."
Mjumbe wa jumuiya ya Wazazi, Hasnata Ramadhani, alieleza malengo ya ziara yao shuleni hapo.
"Tumeamua kupanda miti kama njia ya kuadhimisha maadhimisho ya wazazi, kuhamasisha jamii kupenda mazingira, na kuwasaidia watoto kupenda masomo wanapokuwa katika mazingira safi na tulivu. Pia tunawahamasisha wazazi kuhakikisha chakula kinapatikana shuleni na kupinga ukatili wa aina yoyote dhidi ya watoto."
Mjumbe mwingine, Abdul Husen, aliongeza kuwa lengo lao ni kushirikiana na wanafunzi na walimu katika kuimarisha mazingira ya shule:
"Tumewaelimisha wanafunzi kuhusu mambo yanayotakiwa na yasiyotakiwa shuleni. Kupitia zoezi la kupanda miti, tunalenga kuboresha mazingira yao ya kujifunzia. Tumewapa msaada wa mchele ili kuunga mkono juhudi za chakula shuleni. Wito wetu kwa wazazi ni kuhakikisha wanashirikiana na watoto wao kwa karibu ili kufuatilia maendeleo yao na kuwasaidia wanapokumbana na changamoto."
Ziara hii ya jumuiya ya Wazazi CCM Kambarage imethibitisha kuwa mshikamano kati ya wazazi, walimu, na wanafunzi ni nguzo muhimu katika kukuza maendeleo ya elimu na mazingira bora ya kujifunzia.
Viongozi hawa wameacha alama isiyofutika kwa kutoa msaada wa hali na mali, huku wakisisitiza mshikamano na ushirikiano wa jamii nzima kwa maendeleo endelevu ya kizazi kijacho.
Mjumbe wa jumuiya ya Wazazi, Hasnata Ramadhani Maige akizungumza.
Mjumbe wa jumuiya ya Wazazi, Hasnata Ramadhani Maige akizungumza.