KAMPENI YA UGAWAJI WA VYANDARUA KWENYE KAYA IMEANZA MKOANI SHINYANGA


Na Mapuli Kitina Misalaba 

Wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kuunga mkono juhudi za serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria kwa kushiriki kikamilifu kwenye kampeni za uhamasishaji na ugawaji wa vyandarua vyenye dawa unaoendelea hivi sasa.

Mratibu wa Kudhibiti Malaria Mkoa wa Shinyanga, Betty Charles, amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha kila mwananchi katika mkoa wa Shinyanga anapata chandarua chenye dawa kwa ajili ya kinga dhidi ya malaria. 

Akitoa elimu kuhusu ugonjwa huo, amesisitiza umuhimu wa kutumia vyandarua na kuchukua hatua za kujikinga ili kupunguza maambukizi.

"Kila mwananchi anapaswa kuhakikisha anatoa taarifa sahihi kuhusu kaya yake ili kufanikisha ugawaji wa vyandarua lengo ni kuhakikisha kila kaya inafikiwa," amesema Betty.

Kwa mujibu wa takwimu, matumizi ya vyandarua vyenye dawa mkoani Shinyanga yamepunguza maambukizi ya malaria kwa asilimia 60 hata hivyo, wananchi bado wanahimizwa kuzingatia usafi wa mazingira kwa kuondoa mazalia ya mbu ili kuongeza ufanisi wa kampeni hiyo.

Shirika la Afya Duniani limeeleza kuwa malaria ni moja ya magonjwa yanayoathiri jamii nyingi barani Afrika, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazoathirika zaidi. 

Katika juhudi za kupambana na hali hiyo, serikali ya Tanzania imeongeza bajeti ya sekta ya afya, ambapo Mkoa wa Shinyanga umepata mgao wa vyandarua zaidi ya milioni moja kwa mwaka 2022.

Mratibu huyo ameongeza kuwa, pamoja na changamoto zinazojitokeza, serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo ili kufanikisha lengo la kutokomeza malaria nchini.


Previous Post Next Post