Na Mwandishi wetu, Misalaba Media
Katika maadhimisho ya miaka 48 ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya
Shinyanga Mjini, Daniel Kapaya, amefanya ziara katika Zahanati ya Kitangili na
Shule ya Msingi Kitangili, akitoa elimu juu ya kupinga ukatili dhidi ya watoto
kwa kushirikiana na viongozi wa jumuiya hiyo kata na matawi.
Kapaya amewataka wazazi kufuatilia maendeleo ya
watoto wao shuleni na kushiriki kuchangia chakula pamoja na sukari, akisisitiza
kuwa kutofanya hivyo kunaweza kuchangia ukatili dhidi yao.
Aidha, amewatahadharisha watoto dhidi ya matumizi ya
simu janja (smartphones), akieleza kuwa yanaweza kuwa chanzo cha ukatili wa
mtandaoni, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji na kudanganywa na watu wasiofaa.
Katika zahanati hiyo, Kapaya na timu yake walipanda
miti na kutoa elimu kuhusu umuhimu wa usalama na ulinzi wa watoto.
Shuleni, amezungumza na wanafunzi na wazazi kuhusu
madhara ya ukatili wa kijinsia, mimba za utotoni, ulawiti, ubakaji, na matumizi
ya dawa za kulevya. Vilevile, alitoa kilo 50 za unga wa mahindi kusaidia lishe
ya wanafunzi.
Amesisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuchangia
maendeleo ya shule badala ya kutegea, akibainisha kuwa kutofanya hivyo ni aina
ya ukatili kwa watoto.
Pia, amewataka wataalamu wa afya kufanya kazi kwa
weledi kwa kuzingatia miongozo na taratibu za utumishi wa umma, akisisitiza
umuhimu wa utoaji wa huduma kwa usawa kwa wananchi wote.
