BAADA ya kushindikana kufanyika kwa uchaguzi wa Mwenyekiti wa Soko la Wakulima Nyashishi wilayani Misungwi kutokana na wafanyabiashara kukoswa imani na wasimamizi wa zoezi hilo hatimaye kura za wazi zilifanyika jana kumaliza mvutano huo.
Kufuatia hatua hiyo ya upigaji kura za wazi siku ya pili baada ya kufutwa kwa zoezi hilo kutokana na malalamiko ya wafanyabiashara, Evarist Kahindi maarufu kama Bulale aliibuka kidedea jana kwa kujinyakulia kura 348 dhidi ya 30 aliyepata mshindi wa pili na hivyo kusababisha shamrashamra na vifijo kwenye soko hilo.
Kahindi aliahidi kuwalipa wafanyabiashara hao kwa utumishi uliotukuka katika kipindi chote cha uongozi wake na kuwashirikisha katika masuala yote yanayohusu masuala ya kazi zao ili waweze kupata maendeleo.
Alisema kutokana na kuwepo kwa migogoro ya muda mrefu ya kiutawala atahakikisha anaongoza kwa kufuata katiba ya umoja wao ili kuepusha changamoto zilizokuwa zikijitokeza na kuwaathiri.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Ntende wilayani Misungwi Lameck Sangija alisema anashukuru uchaguzi umefanyika kwa amani na utulivu na kupatikana Mwenyekiti waliyemtaka wafanyabiashara katika soko hilo.
Alitoa wito kwa kiongozi aliyechaguliwa kutimiza wajibu wake wa kuwatumikia wafanyabiashara kwenye soko hilo maarufu kwa wakulima.
Naye Bety Nzigula mfanyabiashara kwenye soko hilo alisema anashukuru kumpata kiongozi ambaye hakujihusisha na utoaji wa rushwa kupata uongozi.
Alisema hilo lilikuwa ndo hitaji lao kumpata kiongozi wa namna hiyo kwani ndo anaweza kuwatumikia watu kwa misingi ya haki na uwazi.
Mfanyabiashara mwingine kwenye soko hilo Japheth Katwale alisema imewachukua muda wa mwaka mzima kukiwepo na mvutano wa kumpata Mwenyekiti baada ya yule wa awali kutolewa na wananchi.
'Mwenyekiti tuliyempata leo ni chaguo la wafanyabiashara na ni mjasiriamali mwenzetu hivyo tumeridhika naye'alisema Katwale.