Na Mapuli Kitina Misalaba
Wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wamehimizwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na
usalama kwa kuhakikisha wanawafahamu majirani zao ili kusaidia kudhibiti
wahamiaji haramu, hususan kuelekea uchaguzi mkuu wa Mwaka 2025.
Akizungumza na Misalaba Media kwa niaba ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga
, Naibu Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Shinyanga, Mrakibu Mwandamizi Lydia
Angumbwike, ameeleza kuwa utaratibu wa kumfahamu jirani ni hatua muhimu katika
kudumisha usalama wa taifa.
"Tunawaomba
wananchi mjue jirani yako, Kila mmoja akiwa na jukumu hili, siyo tu atalinda
usalama wake binafsi, bali pia atasaidia kulinda usalama wa taifa."
amesema Angumbwike.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2024, jumla ya
wahamiaji haramu 3,263 walikamatwa katika Mkoa wa Shinyanga ambapo Wilaya ya
Kahama iliongoza kwa kukamata wahamiaji haramu 841, huku Wilaya za Shinyanga na
Kishapu wahamiaji haramu 1,422 waliokamatwa.
Lydia Mwamsiku ameeleza kuwa Mkoa wa Shinyanga chini ya Afisa
Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Mwandamizi Emmanuel Kajulwa, umeandaliwa
mkakati maalum ili kuongeza usimamizi na kudhibiti wahamiaji haramu katika mkoa
huo.
“Tunaandaa
semina maalum kwa wenyeviti wa vijiji, vitongoji, na wenyeviti wa mitaa kwa
lengo la kuwapa mafunzo ya namna ya kutambua na kudhibiti wahamiaji haramu,”
amesema Lydia.
Aidha, amesema kuwa maafisa wa uhamiaji watapelekwa
kwenye kata mbalimbali mkoani Shinyanga kwa ajili ya kutoa elimu na
kushirikiana na viongozi wa ngazi za kata.
Pia, serikali imejipanga kuimarisha ukaguzi katika
mipaka na kufanya doria za mara kwa mara, hususan katika Wilaya zenye shughuli
nyingi za kilimo kama Ushetu, ambapo hutegemewa vibarua wengi wa msimu.
Vibali Maalum kwa wakulima na wafanyabiashara
wanaohitaji kuajiri vibarua kutoka nje ya nchi, Lydia ameeleza kuwa vibali maalum
vinatolewa kwa gharama nafuu ambapo Shilingi elfu 30 kwa miezi mitatu na elfu
60 kwa miezi sita.
Afisa huyo amesisitiza kuwa sheria kali zimewekwa
kwa watu wanaosaidia wahamiaji haramu kuingia au kuishi nchini.
"Mtu
akikutwa ametoa hifadhi, amempangisha nyumba, au amembeba kwenye gari lake,
huyo mtu atashitakiwa," adhabu yake ni kifungo cha miaka 20 au faini ya
Shilingi milioni 20. pia, vyombo vilivyotumika, kama magari au pikipiki,
vitataifishwa na kuwa mali ya serikali”.amesema Lydia
Wakizungumza na Misalaba Media Mwenyekiti wa mtaa wa
Mitimirefu Bwana Nassoro Warioba na Mtendaji wa Mtaa wa Mitimirefu Bi.
Amgelight Emmanuel Mwanri, wameeleza juhudi zao katika kukabiliana na wahamiaji
haramu huku wakisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wananchi katika kutoa
taarifa za watu wanaoshukiwa kuwa wahamiaji haramu.
Mwaka 2025 unapoelekea uchaguzi mkuu, wananchi wa
Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kufanya kaulimbiu ya "Mjue Jirani Yako"
kuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Niaba ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga , Naibu
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Shinyanga, Mrakibu Mwandamizi Lydia Angumbwike
Mwamsiku, akizungumza na Misalaba Media ofisi kwake leo Januari 23, 2025.
Niaba ya Afisa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga , Naibu
Afisa Uhamiaji wa Mkoa wa Shinyanga, Mrakibu Mwandamizi Lydia Angumbwike
Mwamsiku, akizungumza na Misalaba Media ofisi kwake leo Januari 23, 2025.