MA YATOA UTABIRI MWELEKEO WA MVUA ZA MASIKA 2025






Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a akizungumza na waandishi wa habari Januari 23, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za masika 2025 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka.

……………..

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa kunyesha katika maeneo mengi ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki pamoja na Mashariki mwa mikoa ya Mara na Simiyu.

Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zikitarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria.

Akizungumza na waandishi wa habari Januari 23, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa utabiri wa mwelekeo wa mvua za masika 2025 Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema kuwa mvua hizo zinatarajiwa kuanza wiki ya Pili au ya tatu ya mwezi Machi mwaka huu.

Amesema mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani zinatarajiwa katika maeneo ya Pwani ya Kaskazini, Kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma na Ukanda wa Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga na magharibi mwa mikoa ya Simiyu na Mara) katika kipindi cha Msimu wa Masika, 2025.

Amesema mwelekeo wa mvua za masika 2025 kwa Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara) pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani zitaanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi Machi na kuisha wiki ya kwanza ya mwezi Mei.

Aidha mikoa ya Pwani ya Kaskazini (kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Dar es Salaam, Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba) inatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi chini ya wastani ambazo zitaanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi Machi na kumalizika wiki ya tatu hadi ya nne ya mwezi Mei.

Pia Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki (mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro), inatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani ambapo zitaanza wiki ya pili hadi ya tatu ya mwezi Machi na kumalizika wiki ya kwanza mwezi Mei.

Ameongeza kuwa ongezeko la mvua hizo zinatarajiwa katika kipindi cha mwezi Aprili sambamba na kutoa angalizo la matukio ya hali mbaya ya hewa ikiwemo vipindi vya mvua kubwa kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani.

Pia, Dkt. Chang’a ametaja athari zinazoweza kujitokeza katika Mvua za Wastani hadi Chini ya Wastani kuwa kupelekea upungufu wa upatikanaji wa maji katika baadhi ya maeneo hasa matumizi ya majumbani, kilimo na ufugaji.

“Vipindi vya unyevu wa kuzidi kiasi pamoja na mafuriko vinaweza kujitokeza na kuathiri ukuaji wa mazao katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za Wastani hadi Juu ya Wastani, wadudu waharibifu na magonjwa ya mimea yanayoendana na hali ya ongezeko la unyevu kama vile ukungu yanatarajiwa kuongezeka na kuathiri mazao kama ndizi, mahindi,mpunga, mihogo na maharage,”amesema.

Aidha amewashauri wakulima kuandaa mashamba, kupanda, kupalilia na kutumia pembejeo husika kwa kuzingatia hali ya unyevu katika udongo, kutumia mbinu bora na teknolojia za kuzuia maji kutuama shambani, kuhifadhi maji shambani, kuzuia mmomonyoko na upotevu wa rutuba kutokana na kutuwamisha maji kwa muda mrefu au mafuriko.

“Wakulima wanashauriwa kutafuta taarifa sahihi kutoka kwa maafisa ugani kwa kuzingatia utabiri wa msimu wa wilaya husika katika kuchagua mbegu na zao sahihi.”amesisitiza.

Amewashauri wakulima na maafisa ugani kuendelea kutumia utabiri wa kila siku na siku kumi ili kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa utabiri wa msimu.
Previous Post Next Post