MABORESHO YAANGALIE UPYA MSAMAHA WA KODI KWA TAASISI ZA DINI ZINAZOTOA HUDUMA ZA KIJAMII


Na Moshi Ndugulile

Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini mkoani Shinyanga, wameshauri kuangaliwa upya kwa suala la msamaha wa kodi kwa taasisi za dini zinazotoa huduma kwa jamii.

Wakitoa maoni na mapendekezo yao kwenye Mkutano wa wadau wa kodi ulioandaliwa na tume ya Rais ya maboresho ya kodi Nchini,viongozi hao wamesema suala la kodi limekuwa changamoto kubwa katika uendeshaji wa taasisi hizo ambazo zimelenga kushirikiana na serikali katika utoaji wa huduma hizo ambazo ni pmoja na Shule,zahanati,vituo vya Afya na hospitali.

Katika mapendekezo yake paroko wa parokia ya Ndembezi jimbo katoliki la Shinyanga Padri Paulo Mahona amesema taasisi hizo hazilengi kupata faida bali ni sehemu ya huduma ambazo ziko kwa ajili ya kupunguza changamoto,na kwamba kiasi kidogo cha pesa kinachopatikana kinachangia kuwezesha shughuhuli za uendeshaji.

“ Kwa kweli sisi taasisi za dini tumeendelea kuzingatia na kutii maelekezo ya serikali katika ulipaji wa kodi,na hatupingi hata kidogo, lakini kero ni moja tu, kwamba taasisi za dini mfano shule na vituo vya afya,kwa kweli kimsingi tunatoa huduma na wala si kwa lengo la kufanya biashara, hatuingizi faida,bali lengo kuu ni kuhudumia jamii na kuisaidia serikali,lakini tunatozwa kodi kubwa na tunalipa kadri Mungu anavyotujalia,kwa sababu ya kuheshimu na kutii mamlaka za serikali,tunashindwa kutimiza wajibu mkubwa zaidi ama kutoa huduma kubwa na yenye ubora zaidi kutokana na tozo hizo,kwa sababu hatukusudii kupata mapato kwa ajili ya biashara,bali ni huduma za elimu na afya, kwa hiyo ninaomba kama itawezekana na nina Imani serikali yetu inaweza kufanya hivyo,kutupatia msamaha wa kodi,ili tuweze kutoa huduma zilizo bora zaidi na kuwasaidia wananchi katika ubora wa huduma hizo” amesema Padri Paulo Mahona

Akizungumza katika Mkutano huo Makamu mwenyekiti wa jumuiya ya maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga Askofu Dkt Emanuel Makala wa kanisa la kkkt,amesema kulipa kodi ni utaratibu unaofahamika, kwa kuwa hata kwenye maandiko matakatifu imeelekezwa.

Askofu Dkt Makala amependekeza msamaha wa kodi utolewe kwa taasisi za dini zinazotoa huduma za kijamii, na kwamba taasisi zinazofanya shughuli za biashara ziendelee kulipa kodi

“kwa sababu maandiko matakatifu yanatuelekeza vizuri kabisa juu ya kodi,kwa sababu yanasema ya kaisari mpe kaisari,naya Mungu mpe Mungu,lakini anasema haki huinua taifa,bali dhambi ni aibu ya watu wote,na asiyefanya kazi asile,katika mwelekeo huo tunakiri kwamba taasisi ya dini inayojishughulisha na Biashara inapaswa kulipa kodi, kwa hiyo katika hoja hiyo tunahitaji elimu zaidi kwa viongozi na taasisi za dini,lakini boresheni uwazi na haki katika taasisi hizi kwa kutambua mchango wake katika utoaji wa huduma za elimu na afya, suala hilo liangaliwe kwa jicho la pekee”, amesema Askofu Dkt Emanuel Makala.

Tume ya Rais ya maboresho ya kodi Nchini,imekutana na wadau wa kodi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii Mkoani Shinyanga wakiwemo viongozi wa dini kwa lengo la kutathimini kero,kupokea maoni,na mapendekezo yanayolenga kuboresha ulipaji wa kodi unaozingatia haki.
Mwisho
Padri Paulo Mahona Paroko wa parokia ya Ndembezi Jimbo katoliki la Shinyanga.








Previous Post Next Post