Ligi Daraja la Tatu ngazi ya mkoa kwa upande wa mpira wa miguu wa wanawake imeanza rasmi Mkoani Geita, ikiwa na hamasa kubwa kwa vilabu vya wanawake kujitokeza kushiriki michuano hiyo. Timu nane tayari zimejitokeza kushiriki katika ligi hiyo, ambayo inatarajiwa kuvutia mashabiki wengi na kuibua vipaji vipya vya wanawake katika mpira wa miguu.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa ligi hiyo, mgeni rasmi na Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoani Geita, Salum Kulunge, alisema lengo kuu la ligi hiyo ni kuhakikisha wanapata bingwa wa mkoa kwa upande wa wanawake. Alisisitiza kuwa ligi hiyo ni fursa kubwa kwa wachezaji kuonyesha vipaji vyao na kukuza soka la wanawake katika mkoa huo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Soka la Wanawake Mkoa wa Geita, Elizaberth Makwenda, alielezea mafanikio yaliyopatikana katika maandalizi ya ligi hiyo, akitaja mojawapo kuwa ni ushiriki wa timu nane, jambo linalodhihirisha mwamko mkubwa wa soka la wanawake katika mkoa huo.
Katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Rich Rise, timu ya Jasper Queens ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Nyankumbu Girls. Makocha wa timu zote mbili, Raphael Ngereja wa Nyankumbu Girls, na Mashaka James wa Jasper Queens walieleza kuwa mchezo ulikuwa wa ushindani mkubwa, huku kila timu ikionyesha kiwango bora cha soka.
Nao manahodha wa timu hizo, Kulwa Mdaki wa Jasper Queens na Lucia Patrick wa Nyankumbu Girls, walitoa maoni yao kuhusu mchezo huo, wakieleza kuwa timu zote zilijiandaa vyema na zinatarajia kuonyesha matokeo bora katika mechi zijazo za michuano hiyo.
Ligi hii inatarajiwa kutoa motisha kubwa kwa wachezaji wa kike na kutoa nafasi ya kukuza vipaji mkoani Geita.