RAIS DKT. SAMIA ANASTAHILI KUWA CHAGUO BORA LA UENYEKITI MKUTANO WA “AFRICA ENERGY SUMMIT”

NA JOHN BUKUKU

Wakati ulimwengu ukiendelea kushuhudia changamoto za nishati safi na endelevu, Tanzania imeibuka kuwa kiongozi wa mfano barani Afrika. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa mstari wa mbele katika juhudi hizi, hatua iliyochangia nchi kupewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati.

Mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Januari 27 na 28, 2025, jijini Dar es Salaam, unatazamwa kama fursa muhimu kwa mataifa ya Afrika kujadili na kuweka mikakati ya pamoja ya kukuza nishati safi na endelevu. Lakini ni nini kimeifanya Tanzania na Rais Dkt. Samia kuwa chaguo bora kwa uenyeji wa tukio hili kubwa?

Ni mwaka mwingine wenye matokeo chanya kwa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia. Tangu aingie madarakani, ameweka nishati katika msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa macho ya kiongozi mwenye maono, amesisitiza uwekezaji mkubwa katika nishati jadidifu kama vile umeme wa maji, jua, upepo, na gesi asilia.

Uwezo wake wa kushirikiana na mataifa mengine katika ngazi ya kikanda na kimataifa umeimarisha nafasi ya Tanzania kama mshirika muhimu wa maendeleo ya nishati. Kupitia diplomasia imara, Rais Dkt. Samia ameweza kuvutia uwekezaji na ushirikiano wa kimkakati, jambo lililofungua fursa nyingi kwa nchi yake.

Kwa mtu yeyote anayezuru vijijini Tanzania, mageuzi yanayoletwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni dhahiri.

Hadi Desemba 31, 2024, jumla ya vijiji 12,301 kati ya 12,318 sawa na asilimia 99.9 vimeunganishwa na umeme hali inayowezesha maendeleo katika sekta za afya, elimu, na kilimo.

Mradi wa Julius Nyerere, unaotarajiwa kuzalisha MW 2,115 za umeme, ni ushahidi wa dhamira ya Tanzania katika nishati safi. Huu ni mradi wa kihistoria ambao sio tu utaimarisha upatikanaji wa umeme nchini, bali pia utachochea ukuaji wa uchumi wa viwanda.

Zaidi ya hayo, Tanzania ni kiongozi katika matumizi ya gesi asilia barani Afrika, ikichangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta ya viwanda ndani na nje ya mipaka yake.

Lakini sio takwimu pekee zinazoshuhudia mafanikio haya. Katika mkoa wa Tabora, wilaya ya Uyui, wakazi wanazungumzia mabadiliko makubwa yanayoletwa na umeme.

Mariam Haruna, mkazi wa Kijiji cha Mabama, alisimulia jinsi umeme ulivyoboresha huduma za afya:

“Awali, tulikuwa tukisafiri umbali mrefu kutafuta matibabu. Lakini sasa, huduma zipo karibu, na vifo vya akina mama vimepungua.”

Dkt. Renatus Mathias, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Hassani Mwakasuvi, alisema:”

Uwepo wa umeme umetuwezesha kutumia vifaa vya kisasa vya matibabu na kutoa majibu kwa haraka. Wagonjwa sasa wanatibiwa kwa wakati.”

Jiji la Dar es Salaam lina miundombinu ya kisasa inayohitajika kwa matukio makubwa ya kimataifa. Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, hoteli za kiwango cha kimataifa, na usafiri bora vinatoa hakikisho kwamba Tanzania iko tayari kwa tukio hili muhimu.

Kwa kuchanganya uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia, mafanikio ya kihistoria katika sekta ya nishati, na utayari wa miundombinu, Tanzania imejidhihirisha kuwa mwenyeji wa hadhi ya juu kwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati.

Mkutano huu si tu unatoa fursa ya kushirikiana kimataifa, bali pia unaitangaza Tanzania kama kiongozi wa mfano katika kukuza nishati safi kwa maendeleo endelevu ya Afrika.
Previous Post Next Post