REA YAENDELEA NA USAMBAZAJI WA MITUNGI YA GESI YA KILO SITA KWA BEI YA RUZUKU WILAYA YA HAI MKOANI KILIMANJARO


📌Mitungi ya gesi ya kupikia 3,255 kusambazwa wilaya ya Hai.

📍Hai

Diwani wa viti maalam Kata Ya Machame Mashariki, tarafa ya Lyamungo Wilaya Ya Hai, Mhe. Hausen Nkya amewaomba Wananchi wa kata ya Machame mashariki na Watanzania kwa ujumla kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhamasisha na kuchochea ajenda ya nishati safi ya kupikia nchini. 

Hayo yamebainishwa leo Januari 30, 2025 na Mhe. Nkya mara baada ya kupokea mradi wa uuzaji wa mitungi ya gesi ya kilo sita kwa bei ya ruzuku kata ya Machame Mashariki wilayani  Hai.

Amesema, Rais Samia amekuja na kampeni hii ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwa na lengo la kuhakikisha watu wanapika katika mazingira salama kiafya na kimazingira ili kuboresha maisha na ustawi wa wananchi.

Mhe. Nkya ameongeza kuwa, suala la Nishati Safi ya Kupikia sasa ni ajenda ya kimkakati na inayotakiwa kupewa kipaumbele na wataibeba katika kuelimisha umma kuhusu matumizi salama ya nishati hiyo. 

Kwa upande wake, Mhandisi wa miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini REA, Gift Kombe amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anapika katika mazingira salama na kwamba hatua hiyo itawezekana kwa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata nishati safi ya kupikia iliyo nafuu  na itumikayo kwa urahisi.

Ameongeza kuwa, mtoa huduma kampuni ya Lake Gas  atahudumia wilaya zilizopo ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa kusambaza mitungi ya kilo sita 19,530 kwa bei ya ruzuku ya shilingi 20,800 pamoja na vifaa vyake katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa miji na katika kila wilaya mitungi 3,255 itasambazwa.

Amezitaja wilaya zitakazonufaika kuwa ni pamoja na Wilaya ya Rombo, Hai, Same, Moshi, Mwanga Na Siha .










Previous Post Next Post