RPC MUTAFUNGWA AKABIDHI BENDERA YA TAIFA KWA SWAT, MASHINDANO YA VIKUNDI VYA KUPAMBANA NA UGAIDI


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbroad Mutafugwa Januari 22, 2025 katika Chuo cha Polisi Wanamaji Mwanza (MPC) kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania amekabidhi Bendera ya Taifa kwa Kikosi Maalum cha Mbinu na Silaha (SWAT) kinachokwenda nchini Rwanda kwa ajili ya mashindano ya Vikundi Maalum vya Kupambana na Ugaidi.

Mashindano hayo yatafanyika kuanzia tarehe 23 hadi 30 Januari 2025 na yatahusisha matukio matatu ambayo ni Mapambano ya Karibu (Assault event), Ulengaji Shabaha (Tactical event) na vikwazo (Obstacles) ambapo jumla ya nchi 14 za ukanda wa EAPCCO zinatarajiwa kushiriki.

Aidha, mashindano hayo yatapamba Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Majeshi ya Polisi wa nchi za Mashariki ya Afrika (AGM) ambao unatarajiwa kufanyika nchini Rwanda kuanzia tarehe 27.01.2025 hadi tarehe 29.01.2025.

Akikabidhi bendera ya Taifa ya Tanzania kwa kikosi hicho kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamanda Mutafungwa amewakumbusha washiriki wa mashindano hayo kuwa Taifa linawatazama hivyo wajitahidi kuliwakilisha vyema na kurudi na ushindi huku wakizingatia kauli mbiu ya Jeshi la Polisi ya Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu.

Hata hivyo, Kamanda Mutafugwa mbali na kuwatakai kila la heri, amewataka kwenda kujituma zaidi kwani hakuna mafanikio bila kujituma sambamba na kuongeza ushirikiano miongoni mwao na washiriki wengine.

"Jeshi la Polisi ni taasisi kubwa na limejijengea heshima kubwa ndani na nje ya nchi, sisi hatuna wasiwasi tunatarajia kuona mnarudi na ushindi hivyo mnatakiwa kuongeza morari" amesema Kamanda Mutafungwa

Kwa upande wake, Mkuu wa msafara wa kikosi hicho maalum Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Aizack Mwakisisile amesema yeye pamoja na timu yake wamejiandaa vizuri na wanamatumaini makubwa ya kurejea nchini wakiwa na ushindi.

Kutoka Dawati la Habari Polisi Mwanza
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Wilbroad Mutafugwa.
Mkuu wa msafara wa kikosi hicho maalum Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Aizack Mwakisisile











 

Previous Post Next Post