Na Gabon Mariba - Mara.
Mbunge wa Jimbo la Butiama na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini ameshiriki Ibada na Mazishi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) Mstaafu Marehemu Jaji Frederick Werema aliyefariki dunia Desemba 30, 2024 na kuzikwa leo Januari 04, 2025 kijijini kwao Kongoto Kata ya Buswahili Wilaya ya Butiama mkoani Mara.
Akitoa salamu za rambirambi Naibu Waziri Mhe. Sagini amesema kuwa Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Damas Ndumbaro anatoa pole kwa waombolezaji na kuwataka wawe na moyo wa subira pia Serikali inaungana na familia katika kipindi hiki kigumu.
"Marehemu alikuwa ni nembo ya Kijiji hiki cha Kongoto mpaka Taifa hivyo Wizara ya Katiba na Sheria ikiongozwa na Waziri wetu tunaungana na familia na jamii kwa ujumla kuomboleza pia kama serikali tunaahidi kumuenzi katika yale mema aliyotuachia katika enzi za uhai wake," amesema Mhe. Sagini.
Aidha Mhe. Sagini ametoa wito kwa familia ya Jaji Werema kuendelea kushirikiana na wasiingie katika migogoro ambayo huwa inajitokeza hasa wanapofikia hatua ya mirathi hivyo wagawane mali kwa upendo na amani.
Baadhi ya Viongozi walioshiriki mazishi hayo ni Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Hamza Johari, MNEC Chacha Gachuma, Mwenyekiti CCM Mara Patrick Chandi, Mkuu wa Mkoa Njombe Mhe. Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Kaimu Mkoa wa Mara Mhe. Said Mtanda, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama Ndg. Christopher Siagi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma kaimu Butiama Mhe. Juma Chikoka na Mariam Sagini akiwakilisha kikundi cha Wake wa Viongozi (Millenium)