SHINYANGA: JESHI LA POLISI LAWAKAMATA WATUHUMIWA WA MAUAJI YA DEREVA MKAZI WA LUBAGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wa mauaji ya dereva aliyefahamika kwa jina la Lazaro, mwenye umri wa miaka 35, ambaye mwili wake ulikutwa ndani ya shimo la choo katika kata ya Lubaga, Januari 18, 2025.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi, marehemu Lazaro aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani kabla ya mwili wake kutupwa shimoni.

“Kabla ya tukio hilo kuna mfanyabiashara anaitwa Yona alifungua kesi ya wizi wa kuaminiwa Januari 16, 2025 dhidi ya huyo aliyekuwa dereva wake ambaye kwa sasa ni marehemu, mlalamikaji alieleza kuwa dereva wake hamuoni na pia gari lake halionekani tangu Januari 14 kwahiyo alizileta hizi taarifa kwetu na ufuatiliaji wa jeshi la polisi ulianza mara moja, ambapo Januari 17, 2025 tulifanikiwa kukamata watuhumiwa wawili wakiwa na gari hilo aina ya Toyota Hiace wakiwa wanajaribu kuvuka mpaka kwenda nchini Kenya katika eneo la Tarimelorya”. amesema Kamanda Magomi.

Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili Januari 17, 2025, wakiwa na gari hilo wakijaribu kuvuka mpaka kuelekea Kenya katika eneo la Tarimelorya. “Tunaendelea na upelelezi wa kina na pindi utakapokamilika, jalada litapelekwa kwa Mwanasheria wa Serikali kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema SACP Magomi.

Kamanda Magomi amelaani vikali kitendo cha mauaji hayo akisema, “Ni kosa kisheria kujichukulia sheria mkononi. Kila mtu ana haki ya kuishi, na sisi Jeshi la Polisi tutahakikisha elimu inatolewa kwa wananchi ili kupunguza makosa ya jinai, hasa mauaji.”

Previous Post Next Post