Chama Cha Wanunuzi wa Pamba nchini (TCA), kimewashauri wakulima wa Pamba kufuata kalenda ya zao hilo ikiwemo kuimarisha palizi na kudhibiti wadudu ili waweze kupata mavuno mengi yatakayoinua vipato vyao.
Aidha, wametakiwa kufuata Ushauri wa wataalamu wa kilimo hasa Maafisa Ugani waliosambazwa na serikali kupitia Mpango wa Jenga Kesho Bora (BBT), ambao wanawatembelea wakulima na kutoa Elimu vijijini.
Hayo yamebainishwa na Katibu wa Chama hicho, Boaz Ogolla wakati akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake ambapo alisema wakulima wanatakiwa kudhibiti mapema magugu yanayoathiri zao hilo.
Ogolla amesema zao la pamba ni mimea kama mimea mingine, hivyo inatakiwa kupaliliwa kwa wakati na mkulima asipofanya hivyo magugu yatashindana, na Pamba haitapata chakula.
"Pamba isipopaliliwa mapema itadumaa sababu haipati mwanga na hewa ya kutosha, Pamba ikipaliliwa mapema itapata rutuba na hata kama kuna mvua kigodo itaenda kwenye zao na siyo kwenye magugu" amesema Ogolla.
Ogolla ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua Pamba cha Alliance ginnery amesema wanaunga mkono jitihada za Serikali ikiwemo matumizi ya Teknolojia za kunyunyizia Pamba pamoja na Mpango wa BBT.
Amesema wilaya za Mkoa wa Simiyu zimeingizwa katika Mpango wa BBT, hivyo anaamini wakulima wataongeza uzalishaji wa Pamba na kujiinua kiuchumi.
Katibu wa Chama hicho, Boaz Ogolla
Katibu wa Chama hicho, Boaz Ogolla