WANAFUNZI ZAIDI YA 150 WA JAMII YA KIFUGAJI WAPATA MISAADA

 

Zaidi ya wanafunzi 150 wa jamii ya kifugaji ya kimasai waishio katika Kijiji cha Kimokouwa,wilayani Longido mkoa wa Arusha wamepatiwa misaada ya vifaa mbalimbali vya shule.

Misaada hiyo imetolewa mwishoni mwa wiki na Shirika la Smile Youth and women Support Organisation la jijini Arusha,lengo ni kusaidia wanafunzi hao wa shule za Msingi na Sekondari ili kupata mahitaji ya muhimu ikiwemo sare na madaftari.

Wakizungumza baada ya kupokea misaada hiyo,mmoja wa wanafunzi hao, Musa Melita,alishukuru wadau hao kwa msaada huo ambao umewawezesha kwenda shule wakiwa na mahitaji yote muhimu kama wanafunzi wengine.

“Tulikuwa na changamoto ya kwenda shule kwa wakati kwa sababu tulikuwa hatuna sare wala mahitaji mengine muhimu kama madaftari ila kwa sasa tunashukuru msaada huu utatuwezesha kwenda shule kwa wakati na tutasoma kwa bidii,”amesema

“Tunaomba wadau wengine watusaidie sisi watoto wa jamii hizi za pembezoni ikiwemo za kifugaji ambazo nyingi tunakumbana na changamoto,tukipata msaada wa mahitaji ya shule itatuwezesha kufanya vizuri darasani,”ameongeza

Naye Losinyati Laizer ambaye ni mmoja wa wazazi wa watoto waliofunaika na msaada huo, amesema hiyo inawapa ari kama wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata elimu.

“Ilikuwa ni ngumu kupata fedha kwa ajili ya kurudisha watoto shule ila tunashukuru wadau kwa kutusaidia,tunazidi kujifunza umuhimu wa kupeleka watoto shule na kuwapatia mahitaji ya muhimu ya kila siku,”ameongeza

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya Msingi Kimokouwa, Sarone Olekuku,alieleza kuwa wanaednelea kupambana kupunguza utoro shule hivyo kwa kisingizio cha kukosa mahitaji muhimu ya shule ikiwemo madaftari.

Awali Mkurugenzi wa shirika hilo,Omega Mlay, amesema kuwa lengo la misaada hiyo ni kuhakikisha wanafunzi hao wa pembezoni wanaoata haki yao ya msingi ya kusoma kama wanavyopata wengine.

“Serikali inatoa elimu bure na sisi kama wadau tunajitahidi kushirikiana kuunga mkono serikali kwa kupatia watoto mahitaji muhimu ya shule ili waweze kuhudhuria masomo kwa wakati na kuepusha visingizio vya ukosefu wa vifaa vya kujifunzia,kwnai tunatamani jamii hizi zipate elimu,”amesema


Mratibu wa zoezi hilo,Elia Mushi alieleza kuwa jamii za pembezoni zimekuwa zikisahaulika na misaada mingi huishia mijini ndiyo maana wao wamejikita kuhakikisha wanatembelea na kusaidia jamii hizo za pembezoni zenye uhitaji.

Misaada iliyokabidhiwa kwa wanafunzi hao ni daftari,penseli,kalamu,sare za shule,mafuta ya kujipaka na vifaa vingine.




Previous Post Next Post