WANANCHI BIHARAMULO WAPATIWA ELIMU KUHUSU MARBURG

  


Na WAF, Biharamulo, Kagera.

Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Uongozi wa Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera leo Januari 23, 2025 wametoa elimu kuhusu jinsi ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya marburg kwa wafanyabiashara katika soko la Biharamulo kufuatia kuripotiwa huo katika Wilaya hiyo.

Mkurugenzi wa Huduma za Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa Sekta inaendelea kuimarisha juhudi za kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu namna ya kujikinga na ugonjwa huo hatari, kusambaza vipeperushi vyenye ujumbe wa tahadhari pamoja na mambango.

Dkt. Kapologwe ambaye aliambatana na Mkuu wa Wilaya hiyo Mhe. SACP Advera John Bulimba, amesema hatua hiyo ni  utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye amesisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari zote zinazohitajika ili kulinda afya ya wananchi.

Dkt. Kapologwe alieleza kuwa Marburg huenezwa haraka kupitia majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa, kama vile damu, matapishi, mate, mkojo, kinyesi, au jasho. 

Amevitaja vyanzo vingine  kuwa ni kugusa vitu vilivyotumiwa na mgonjwa wa Marburg au kula mizoga ya wanyama walioambukizwa, kama popo, nyani, tumbili, na sokwe.

"Dalili  kuu za ugonjwa wa Marburg ni pamoja na homa kali, kuumwa kichwa, kutapika au kutapika damu, kuharisha au kuharisha damu, na kutokwa na damu katika sehemu mbalimbali za mwili," amefafanua Dkt. Kapologwe.

Dkt. Kapologwe ametoa wito kwa wananchi kuchukua hatua za kujikinga na ugonjwa huu kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya, ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara, kuepuka kugusa majimaji ya mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Marburg, kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono, kukumbatiana, au kubusiana, kuepuka kula au kugusa mizoga ya wanyama kama popo, nyani, na tumbili na kuepuka kugusa au kuosha maiti ya mtu aliyefariki akiwa na dalili za Marburg, na kusisitiza jamii kutoa taarifa kwa wataalam wa afya ili mazishi yafanyike kwa kuzingatia kanuni za afya na utu.

Aidha, Dkt. Kapologwe amewahimiza wananchi kutoa taarifa haraka kwa kupiga simu namba 199 bila malipo endapo wataona mtu mwenye dalili zinazofanana na Marburg.

Hatua hizi zote zinalenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa salama na kuzuia maambukizi zaidi ya ugonjwa huo hatari.

Kwa upande wake Mhe. SACP  Bulimba amepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na Serikali pamoja na Wadau kwa kufika Biharamulo kwa ajili ya kutoa huduma za tiba, kinga pamoja na elimu ya afya huku akiwataka wananchi kuzingatia kanuni za afya ili  kuepukana na magonjwa.









Previous Post Next Post