BAADHI ya shule binafsi Jijini Mwanza wamesema kuwa pamekuwepo na kusuasua kwa ulipaji wa ada mwanzoni mwa mwaka baada sherehe za krismas na mwaka mpya kutokana na wazazi wengine kuleta watoto wao bila malipo.
Hayo yamebainishwa na walimu wa shule hizo kwa nyakati tofauti jana katika Jijini Mwanza baada ya kufunguliwa kwa shule za msingi na sekondari.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Saana English Medium alisema wanakabiliana na changamoto ya wazazi wengi kutolipa ada katika kipindi cha mwanzo wa mwaka akihusisha hali hiyo na sikukuu ya krismas na mwaka mpya kuchangia hali hiyo.
Alisema wanafunzi wanaosoma hapo wanaoletwa bila ada wanawapokea ili waendelee na masomo yao kuwaepusha kuwa nyuma kwenye silabusi wanayosoma.
Wakati huo huo Mkurugenzi wa shule hiyo David Katunge alisema kuwa shule yao itaendelea kuwapokea wanafunzi bila kubagua wale ambao hawajalipiwa ada kutokana na uhusiano mzuri baina yao na wazazi.
Mkurugenzi huyo ambaye vilevile ni Mkurugenzi wa EDIM Land and Engineering Consult (T) aliwasihi wazazi wa wanafunzi kuhakikisha kuwa wanapimiwa ardhi zao na kupata hati miliki kwani wanaweza kutumia kuchukua mikopo ya kusomeshea watoto wao.
Katunge alisema mwananchi anapokuwa amepimiwa ardhi yake anakuwa na fursa ya kutumia katika mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuwasaidia kujiendeleza kiuchumi hivyo kuwa katika mazingira mazuri hata ya kumudu kugharamia masomo ya watoto wao.
Naye Mchungaji wa Kanisa la AICT Joseph Iseme ambaye anafundisha wanafunzi masomo ya dini kwenye shule hiyo alisema kuwaandaa wanafunzi mapema kunasaidia kuwajenga kiroho watoto na hivyo kuwa watu wema kwenye jamii.
Alisema wanafunzi wanapokuwa na elimu ya dini inawasaidia kuwa jitihada ya kujifunza kwa bidii masomo yao.