WAZIRI KOMBO AAGANA NA BALOZI WA MAREKANI

 

Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano kwa Ubalozi wa Marekani nchini na kuahidi kumpatia ushirikiano wa karibu Balozi ajaye katika utekelezaji wa majukumu yake awapo Tanzania pamoja na kuangazia maeneo ya kuongeza wigo wa ushirikiano kwa manufaa ya nchi zote mbili.


Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo, akimuaga Balozi wa Marekani nchini, Mhe. Michael Battle anayetarajiwa kuondoka nchini hivi karibuni.

Waziri Kombo amemshukuru Balozi Battle kwa ushirikiano mzuri kati ya wizara na ubalozi katika kipindi chote cha uongozi wake pamoja na kufanya kazi kwa karibu na sekta na wizara mbalimbali za kimaendeleo nchini.

Aidha, ametumia fursa hii kutoa salamu za pole kwa msiba wa Rais Mstaafu wa Marekani, Hayati Jimmy Carter aliyefariki Dunia Desemba 29, 2024.

Kwa upande wake, Balozi Battle amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira yake katika kuleta maendeleo Tanzania lakini pia kwa utayari wake katika shughuli za ushirikiano.

Ameomba pia Wizara kumpa ushirikiano wa karibu Kaimu Balozi atayekuwepo wakati Marekani ikingoja kutuma Balozi mwingine.
Previous Post Next Post