Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Mitume na
Manabii Kanda ya Ziwa Nabii Meshack Mpanduji, amezindua rasmi maombi maalumu
yanayotambulika kwa jina la Maombi ya Nguvu Kubwa Kila Mahali.
Uzinduzi huo umefanyika katika Kanisa la Jehovah
Shalom lililopo Kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga.
Maombi hayo yamelenga kuimarisha huduma tano za
kiroho zinazojumuisha Mitume, Manabii, Wainjilisti, Wachungaji, na Walimu wa
makanisa.
Katika mahubiri yake, Nabii Meshack amewahimiza
Watanzania kuepuka kufanya mambo kwa mazoea au kwa kuiga, akisisitiza kuwa mara
nyingi watu wanaofanya vitu bila uelewa hufeli.
“Jambo lolote unalolifanya hakikisha
unauelewa kama hauna uelewa, usilifanye. Unapotaka kuanzisha biashara yoyote,
jitahidi kuielewa kwanza watu wengi wanashindwa kwa sababu wanajiingiza kwenye
mambo bila kuwa na maarifa ya kutosha.”
Katika hatua nyingine, Nabii Meshack amezungumzia
masuala ya ndoa na umuhimu wa kujiandaa kiakili na kiroho kabla ya kuingia
kwenye ndoa.
“Kwenye kutengeneza mji, kuna msichana
na mvulana, na kuna mwanamke na mwanaume. Msichana hatimizi hatima ya ndoa;
anayetimiza hatima ya ndoa ni mwanamke. Maandiko yanasema mtu atamwacha baba na
mama na kuambatana na mke, siyo msichana. Hali kadhalika, mvulana hatimizi
hatima ya ndoa, bali mwanaume ndiye mwenye wajibu huo.”
Ameeleza kuwa migogoro mingi ya ndoa hutokea kwa
sababu wanandoa huingia kwenye maisha ya ndoa wakiwa hawajajitambua vya
kutosha.
“Wanaotaka kuingia kwenye ndoa,
jichunguzeni kwanza. Kama wewe ni msichana, bado hujawa tayari kuwa mke. Vivyo
hivyo, kama bado ni mvulana, usilazimishe kuingia kwenye ndoa.”
Baadhi ya waumini waliohudhuria uzinduzi huo
wameeleza kufurahishwa na mahubiri ya Nabii Meshack, hasa katika suala la ndoa,
wakisema yamewapa mwanga wa kutambua majukumu yao katika maisha ya ndoa.
Mwenyekiti wa Mitume na Manabii Mkoa wa Shinyanga,
Aposto Themistocles Paul, amesema kuwa maombi hayo yatakuwa na nguvu kubwa na
yatafanyika kwa vitendo.
“Kuanzia sasa, tutafanya maombi haya
nyumba kwa nyumba, kanisa kwa kanisa, na kila wilaya ili kuombea wenye
changamoto mbalimbali.”
Ameongeza kuwa wanatarajia kuandaa maombi maalum kwa
ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ili kuombea amani ya Tanzania.
“Tunashauri watu waendelee kuwa na vyama
vyao vya siasa lakini kudumisha umoja na amani. Tanzania ni nchi yetu sote,
hivyo tuilinde kwa maombi.”
Katibu wa Baraza la Mitume na Manabii Mkoa wa Shinyanga,
Nabii Avithi Salvatory, ambaye pia ni Kiongozi wa Kanisa la Jehovah Shalom,
amesema kuwa lengo la uzinduzi wa Nguvu Kubwa Kila Mahali ni kuwafikia
watu wengi na kuombea taifa pamoja na viongozi wake.
“Tutamwombea Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, pamoja na wasaidizi wake wote ili waendelee
kuongoza kwa hekima na busara.”
Maombi hayo yatajikita katika maeneo mbalimbali
muhimu, ikiwemo kukemea ukatili unaoendelea katika jamii, kuombea uchumi wa taifa
na ustawi wa watu binafsi, kuombea amani ya taifa, kuomba dhidi ya vitendo vya
uovu vinavyofanyika kinyume cha utaratibu wa nchi.
Mwenyekiti wa Mitume na Manabii Mkoa wa Shinyanga,
Aposto Themistocles Paul akizungumza katika uzinduzi huo wa Nguvu kubwa kila
mahali.
Katibu wa Baraza la Mitume na Manabii Mkoa wa Shinyanga,
Nabii Avithi Salvatory, ambaye pia ni Kiongozi wa Kanisa la Jehovah Shalom
akizungumza kwenye uzinduzi wa Nguvu kubwa kila mahali.
Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Mitume na
Manabii Kanda ya Ziwa Nabii Meshack Mpanduji akihubiri leo Februari 10, 2025.
Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Mitume na
Manabii Kanda ya Ziwa Nabii Meshack Mpanduji akihubiri leo Februari 10, 2025.
Post a Comment