WILAYA ya Nyang'hwale imeazimisha kwa namna yake miaka 48 ya kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambapo ujenzi wa ofisi ya tawi ilichangiwa fedha taslimu, upandaji miti na uchimbaji msingi ulifanywa na wananchi kuenzi kuasisiwa kwa chama hicho
Maadhimisho hayo ambayo yalifanyika jana katika Kijiji Cha Ifugandi iliyopo kata ya Busolwa yaliongozwa na Mwenyekiti wa Chama wa wilaya hiyo Alhaji Mtole ambapo walianza kwa zoezi la upandaji miti zaidi ya 150 na uchimbaji msingi wa ofisi ya chama ya kitongoji katika eneo hilo.
Mtole alisema wanachama wanayo majukumu ya kuhakikisha kuwa wanakijenga chama wenyewe kama ambavyo Mwenyekiti wa CCM Dk Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza.
Aidha Mtole aliongoza kampeni ya kuchangia ujenzi wa ofisi ambapo zaidi ya shilingi 250,000 zilichangwa papo kwa papo na kutolewa ahadi ya ununuzi wa bati zote za kuezekea ofisi hiyo na Mbunge wa Jimbo la Nyang'hwale Hussein Kasu.
Wakati huo huo wanachama watatu toka vyama vya upinzani walijiunga na CCM wakisema wamefurahishwa na kazi kubwa iliyofanywa na serikali katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati hapa nchini.
Naye Mbunge wa Jimbo hilo Hussein Kasu alishukuru serikali ya awamu ya sita kwa namna ilivyosaidia maendeleo ya kijamii katika eneo hilo ambapo miradi mbalimbali kwenye sekta ya elimu, afya, maji na miundombinu imetekelezwa kwa ufanisi mkubwa.
Kasu alitaja ongezeko la shule za sekondari kutoka tisa hadi 18 na za msingi kutoka 55 hadi 75, Kidato cha tano na sita kutoka mbili hadi tano,vituo vya viwili sasa viwili hadi vitano,zahanati 25 hadi 37 na zaidi asilimia 75 upatikanaji wa maji.
Diwani wa Kata hiyo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Revocatus Jacob alishukuru serikali kwa kuwezesha eneo hilo kujengewa shule ya sekondari kwa masomo ya kidato cha tano na sita.
Alisema uamuzi wa sherehe hizo kufanyika katika kata yao ni faraja kwa wananchi wa eneo hilo kwani wameweza kufahamu kwa kina kuhusu chimbuko la chama chao na malengo yake mahususi katika kuwatumikia watanzania.