" DIWANI ZAMDA SHABAN AFANYA MKUTANO WA HADHARA, MNADA MPYA KUZINDULIWA KATA YA NDALA WANANCHI WAPONGEZA

DIWANI ZAMDA SHABAN AFANYA MKUTANO WA HADHARA, MNADA MPYA KUZINDULIWA KATA YA NDALA WANANCHI WAPONGEZA

Na Mapuli Kitina Misalaba

 Diwani wa Kata ya Ndala ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Zamda Shaban, ametangaza kuwa mnada mpya wa vitu mbalimbali, ikiwemo nguo, mboga mboga na biashara ndogondogo, utafanyika rasmi kuanzia Jumatano ijayo.

Ameyasema hayo kwenye mkutano wake wa hadhara Februari 26, 2025 ameeleza kuwa mnada huo utakuwa unafanyika kila Jumatano kuanzia asubuhi, ambapo amewakaribisha wafanyabiashara na wajasiriamali kupeleka bidhaa zao na kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi.

Akizungumza na wananchi wa kata hiyo, Mhe. Zamda amesema kuwa uamuzi wa kuanzisha mnada huo umetokana na juhudi zake kwa kushirikiana na viongozi wengine wa kata katika kutafuta njia za kukuza uchumi wa eneo hilo, hasa baada ya kuona kwamba soko la Ndala limekuwepo kwa zaidi ya miaka 21 bila kuwa na maendeleo makubwa.

"Tumekaa kama viongozi tukafikiria, soko letu la Ndala limekuwepo kwa muda mrefu lakini halijapata ufumbuzi wa kudumu. Kwa sasa tumejipanga kuhakikisha linakuwa sehemu ya kukuza uchumi wa wakazi wa Ndala," amesema Mhe. Zamda.

Ameeleza kuwa baada ya kufuatilia suala hilo, alilipendekeza kwa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kupata kibali kutoka kwa Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Manispaa kuendelea na taratibu za kuanzisha mnada.

"Katika eneo letu la Soko la Ndala kumekuwa na changamoto nyingi. Wafanyabiashara walikuwa wanashindwa kukaa kwa muda mrefu, lakini sasa tumepata suluhisho. Eneo letu la chama cha mapinduzi pia tumeliomba na sasa linaenda kuwa sehemu ya mnada huu mpya. Mnada huu utafanyika Jumatano kwa kuwa hakuna mnada mwingine siku hiyo," amesema Zamda

Amefafanua kuwa mnada huo utakuwa fursa muhimu kwa wafanyabiashara wa bidhaa mbalimbali kama mitumba, matunda, na huduma za chakula.

"Mitumba ya grid one itakuwa sehemu ya mnada huu, naomba wanandala tuwape nafasi wafanyabiashara wa mnada waje ili kuinua uchumi wa kata yetu. Wananchi kutoka kata nyingine jirani pia wanakaribishwa kushiriki," amesema Zamda.

Baadhi ya wananchi wa Kata ya Ndala wameeleza kufurahishwa na hatua hiyo, wakisema kuwa mnada huo utachochea ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja, kata na Manispaa ya Shinyanga kwa ujumla.

Pia wamesema kuwa mnada huo utafungua fursa za ajira kwa vijana na wanawake wajasiriamali.

Mkutano huo wa hadhara umewakutanisha wananchi na viongozi wa taasisi mbalimbali kama SHUWASA, TANESCO, Idara ya Ardhi na TARURA ambapo wananchi wamepata nafasi ya kuuliza maswali kuhusu changamoto zinazowakabili, ambapo wataalamu wa taasisi husika wamejibu na kutoa ufafanuzi.

Diwani huyo ametolea ufafanuzi kuhusu maoni ya wananchi juu ya changamoto za miundombinu ya barabara na huduma za afya akieleza kuwa serikali inaendelea kushughulikia masuala hayo, huku akiwataka wananchi kuwa wavumilivu wakati suluhisho la kudumu likitafutwa.

Mnada wa Ndala unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya kiuchumi katika Manispaa ya Shinyanga, huku ukitoa fursa kwa wakazi wa Ndala na maeneo jirani kunufaika na biashara mbalimbali.Diwani wa Kata ya Ndala ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Zamda Shaban, akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara Februari 26, 2025.Diwani wa Kata ya Ndala ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Zamda Shaban, akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara Februari 26, 2025.Diwani wa Kata ya Ndala ambaye pia ni Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Mhe. Zamda Shaban, akizungumza kwenye mkutano wake wa hadhara Februari 26, 2025.

Mkazi wa kata ya Ndala akitoa maoni yake kwenye mkutano wa hadhara ambao umeandaliwa na Diwani wa kata hiyo Mhe. Zamda Shaban.

Post a Comment

Previous Post Next Post