" DKT LUZILA: TUMEBORESHA ZAIDI KITENGO CHETU CHA HUDUMA KWA WATEJA HOSPITALI YA RUFAA MKOA SHINYANGA, PONGEZI ZIMEONGEZEKA

DKT LUZILA: TUMEBORESHA ZAIDI KITENGO CHETU CHA HUDUMA KWA WATEJA HOSPITALI YA RUFAA MKOA SHINYANGA, PONGEZI ZIMEONGEZEKA


Na George Mganga, Shinyanga RRH

HOSPITALI ya Rufaa Mkoa Shinyanga kupitia Kitengo cha Huduma kwa wateja, imeendelea kuboresha huduma zake kwa kuhakikisha inajali zaidi maslahi ya wagonjwa wanaofika kuhudumiwa.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani, Luzila John, amesema kitengo hicho kwa sasa kimetoa fursa kwa wateja kutoa maoni, malalamiko, kero na hata pongezi zao zenye lengo la kuboresha zaidi utoaji wa huduma.

Kupitia fursa hiyo, maoni, kero na pongezi ambazo hutolewa na wateja huratibiwa na kitengo kisha hufikishwa katika timu ya uongozi wa hospitali kwa ajili ya kufanyiwa kazi, na kwa mtumishi atakayebainika kwenda kinyume na miongozo, huchukuliwa hatua za kinidhamu kwa haraka.

“Kitengo chetu cha huduma kwa wateja kimeimairika zaidi kwa sasa, malalamiko ambayo tulikuwa tukipokea miaka ya nyuma ni tofauti na sasa, pongezi zimeongezeka.

“Fursa tuliyowapa wateja wetu kwa sasa wanaweza kutoa maoni, kero, malalamiko na hata pongezi ambazo hufikishwa sehemu ya utawala kisha kufanyikwa mchakato na kuchukua hatua kwa wale watakaobainika kuwa sehemu ya tatizo au kero kwa wagonjwa”, amesema Dkt. Luzila.

Aidha, kwa upande wake Bi. Joyce Kiberiti ambaye ni Mkuu wa Kitengo hicho, amesema Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga imekuwa ikipokea pongezi nyingi kipindi hiki, tofauti na miaka ya nyuma, akieleza imechagizwa na huduma hususani za kibingwa.

Amesema huduma zimekuwa zikitolewa kwa kuzingatia miongozo ya afya na serikali kwa ujumla, lakini vilevile kitengo kupitia maoni ya wateja kimekuwa kikiyafanyia kazi kwa kuchukua hatua kwa watumishi wasiozingatia maslahi ya wateja.

“Sisi tunajali zaidi maslahi ya wateja wetu, hospitali yetu imekuwa na huduma nzuri, hizi huduma za kibingwa zimechagiza zaidi kupata pongezi nyingi.

“Ukipita katika maeneo mbalimbali ya hospitali, tumeweka matangazo yenye namba za viongozi wa hospitali lakini vilevile namba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, ambazo zinawapa nafasi wateja wetu kupiga moja kwa moja pindi wanapopata changamoto”, amesema.

Kando na hayo, Bi. Kiberiti amewahakikishia wananchi kuwa huduma katika Hospitali ya Rufaa Mkoa Shinyanga zimeimarika zaidi na huduma zinazotolewa ni nzuri na zinawapa kipaumbele kikubwa wateja, amewataka wananchi kuendelea kufika hospitali kwa ajili ya kupata vipimo mbalimbali kwa lengo la kustawisha maendeleo ya afya zao.

Post a Comment

Previous Post Next Post