Na Mapuli Kitina Misalaba
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linaendelea na
uchunguzi wa mauaji ya mtoto Dorin Almin (7), mwanafunzi wa darasa la pili
katika Shule ya Msingi Msufini, ambaye aliuawa na mtu au watu wasiojulikana
katika mtaa wa Mlepa, kata ya Ndala, Manispaa ya Shinyanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna
Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Janeth Magomi, amesema tukio hilo liliripotiwa
mnamo Februari 11, 2025, majira ya saa 12 jioni na mzazi wa marehemu, Aminiel
Benard.
"Tulipata
taarifa kutoka kwa mama wa mtoto ambaye aligundua kuuawa kwa mtoto wake wa
kike. Mtoto huyo alikuwa akiishi na bibi yake katika kitongoji cha Msufini,
kata ya Ndala. Aliondoka kwenda shule lakini hakurejea, hali iliyopelekea bibi
yake kuanza kumtafuta jioni hiyo," amesema Kamanda
Magomi.
Jeshi la Polisi tayari linamshikilia mtuhumiwa mmoja
wa kiume kwa ajili ya mahojiano, huku uchunguzi ukiendelea. Inadaiwa kuwa mama
mzazi wa marehemu anaishi Bugweto baada ya kuolewa na mwanaume mwingine, na
mmoja wa watu wanaoshikiliwa ni aliyekuwa mume wake.
"Sisi
kama Jeshi la Polisi tutaendelea na upelelezi wa kina ili kubaini wahusika wa
mauaji haya na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake,"
ameongeza Kamanda Magomi.
Kwa upande wao, familia ya marehemu imeeleza
kusikitishwa na tukio hilo, huku wakazi wa Ndala wakilitaka Jeshi la Polisi
kufanya uchunguzi wa kina ili wahusika wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Mwenyekiti wa mtaa wa Mlepa, Abel Baziri, amesema
kuwa kwa kushirikiana na jeshi la sungusungu, wamejipanga kuchukua hatua za
kuimarisha ulinzi, ikiwemo kufanya doria na misako ya nyumba kwa nyumba ili
kubaini wageni waliowasili kwenye mtaa huo bila taarifa rasmi kwa serikali ya
mtaa.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini
wahusika wa tukio hilo la kikatili.
TAZAMA VIDEO
Post a Comment