" JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAANZA ZIARA, YAWAHIMIZA WAZAZI KUIMARISHA MALEZI YA WATOTO

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAANZA ZIARA, YAWAHIMIZA WAZAZI KUIMARISHA MALEZI YA WATOTO

Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imeanza ziara rasmi ya kutembelea kata zote 17 za jimbo la Shinyanga Mjini ambapo leo imetembelea kata ya Mwamalili na kata ya Old Shinyanga ndani ya Manispaa ya Shinyanga.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mzee Fue Mrindoko, amesisitiza umuhimu wa malezi bora kwa watoto na kuonya dhidi ya mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanalea watoto wao kwa maadili mema ili kuwaepusha na vitendo visivyofaa kama vile wizi, ukahaba, na utumiaji wa madawa ya kulevya.

Aidha, Mrindoko amekemea vikali ukatili dhidi ya wanawake na watoto, akiwataka wanaume wanaojihusisha na vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa imani za kishirikina kuacha mara moja tabia hizo huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuchukua hatua kali kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo.

Mwenyekiti huyo pia amekemea ushoga kwa wanaume na kuwataka wanawake wanaouza miili yao kwa tamaa ya pesa kuachana na tabia hiyo ambapo ameeleza kuwa vitendo hivyo ni dhambi kwa Mwenyezi Mungu na vinakiuka maadili ya taifa la Tanzania.

Katika ziara hiyo, Mrindoko ametumia nafasi hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa changamoto zinazowakabili, hususan tatizo la upatikanaji wa umeme na maji katika kata ya Mwamalili, zitashughulikiwa kwa usimamizi wa CCM na serikali ya awamu ya sita.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Yotham Kibabi, amewahimiza wanachama wa jumuiya hiyo kuongeza wanachama wapya.

Amesisitiza pia umuhimu wa kulipa ada za uanachama kwa wakati ili wanachama waendelee kuwa hai ndani ya CCM.

Jumuiya hiyo imeendelea kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Shinyanga Mjini.

Viongozi wa jumuiya hiyo wameendelea kuahidi kumuunga mkono katika hatua zote za maendeleo na kuhakikisha anashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Mhandisi James Jumbe, ameeleza imani yake kuwa CCM itashinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 huku akitoa wito kwa wanachama na viongozi wa chama kuendelea kudumisha mshikamano ili kuhakikisha ushindi wa CCM.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mhandisi Jumbe amesema kuwa Rais Samia ameonyesha uongozi thabiti na mafanikio makubwa katika sekta muhimu kama vile miundombinu, elimu, afya, na utoaji wa mikopo kwa makundi maalum.

"Rais Samia ni mtu wa maendeleo, ameboresha miundombinu ya barabara ambayo inasaidia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi yetu," amesema Mhandisi Jumbe.

Amesema Rais Samia amefanya juhudi kubwa katika sekta ya afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba, ujenzi wa hospitali, vituo vya afya, na zahanati. Vilevile, ameboresha sekta ya elimu kwa kuongeza mikopo ya wanafunzi wa vyuo vikuu na kuajiri walimu kwa wingi.

Mhandisi Jumbe amewahimiza wanachama wa CCM kushirikiana kwa nguvu, kujenga chama, na kumuunga mkono Rais Samia pamoja na viongozi wa chama ili kuhakikisha ushindi  katika uchaguzi wa mwaka 2025.

"Tushirikiane kwa nguvu, tuendelee kujenga chama, tuunge mkono Rais wetu na viongozi wa chama, na tupate ushindi mkubwa," amesema Jumbe.

Mjumbe huyo wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini pia ameeleza kuwa utendaji wa Rais Samia katika utekelezaji wa Ilani ya CCM umekuwa wa kiwango cha juu huku akitaja kuwa ndiyo  sababu wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM walimpendekeza kwa kauli moja kuwa mgombea pekee wa urais kupitia chama hicho katika uchaguzi mkuu wa 2025.

"Mheshimiwa Rais Samia anatekeleza majukumu yake kwa weledi mkubwa, ndiyo maana wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM walipitisha azimio la kumpitisha kuwa mgombea pekee wa Urais kupitia CCM," amesema Jumbe.

Pia amempongeza Dkt. Emmanuel Nchimbi kwa kuteuliwa kuwa mgombea mwenza, akisema kuwa ni mtu mwenye heshima, mchapakazi, na mstahimilivu.

"Kwa hiyo ukiangalia muunganiko wa Dkt. Samia na Dkt. Nchimbi, hakuna mashaka kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka huu, tunaenda kushinda kwa kishindo," ameongeza Jumbe.

Baadhi ya wanachama wa Jumuiya hiyo wamepongeza ziara hiyo na kuahidi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali na CCM ambapo wamesema kuwa ziara kama hizo zinawapa fursa ya kuelewa mipango ya maendeleo na kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.

Wajumbe wengine wa kamati ya utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga ambao wameshiriki kwenye ziara ya leo ni pamoja na Daniel Kapaya, Marry Makamba na Zulfa Hassan.

Ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini inaendelea kesho kwa kutembelea kata nyingine ndani ya jimbo hilo.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko akizungumza kwenye katika kata ya Mwamalili ikiwa ni sehemu ya ziara ya jumuiya hiyo leo Februari 18, 2025.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Doris Yotham Kibabi, akihimiza wanachama wa jumuiya hiyo kuongeza wanachama wapya. 

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini Mhandisi James Jumbe, akizungumza kwenye ziara hiyo leo Februari 18, 2025.

 


 

Post a Comment

Previous Post Next Post