" JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAENDELEA NA ZIARA YA KUTATHMINI MAENDELEO YA ILANI, WAZAZI WAHIMIZWA KUCHANGIA CHAKULA SHULENI ILI KUONGEZA UFAULU

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAENDELEA NA ZIARA YA KUTATHMINI MAENDELEO YA ILANI, WAZAZI WAHIMIZWA KUCHANGIA CHAKULA SHULENI ILI KUONGEZA UFAULU

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini Mzee Fue Mrindiko, amewahimiza wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika zoezi la uchangiaji wa chakula shuleni kwa ajili ya watoto wao ili kuimarisha afya zao na kuongeza ufaulu.

Mrindiko ametoa wito huo wakati wa ziara ya jumuiya hiyo inayoendelea katika kata zote 17 za Jimbo la Shinyanga Mjini, ambapo leo Februari 19, 2025, wamefanya ziara katika Kata ya Kizumbi na Kitangili.

Mrindoko amesisitiza umuhimu wa wazazi kuhakikisha wanachangia chakula shuleni ili wanafunzi waweze kusoma kwa utulivu bila changamoto za njaa.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kulaani vikali vitendo vya ukatili dhidi ya watoto, hasa ulawiti na ubakaji, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuwachukulia hatua kali wahusika wa matukio hayo.

Katika ziara hiyo, Diwani wa Kata ya Kizumbi, Reuben Kitinya, ameishukuru Serikali kwa kutoa shilingi milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya sekondari, akisema itasaidia kupunguza umbali wa kilomita 12 ambao wanafunzi walikuwa wakitembea hadi Shule ya Sekondari Kizumbi.

Ameeleza kuwa shule hiyo mpya, Sekondari ya Igalukilo, inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi Machi 2025 kutoka shule za msingi Mwamashele, Lyandu, na Bugayambele.

Kwa mujibu wa Msimamizi wa Ujenzi wa Shule ya Sekondari Igalukilo, Maliki Yazidi Nofel, ujenzi wa shule hiyo ulianza Septemba 1, 2024, na ulipaswa kukamilika Desemba 30, 2024, lakini umekumbwa na changamoto za mkandarasi.

Amebainisha kuwa madarasa mapya yako tayari kutumika, huku maabara tatu, maktaba, na jengo la kompyuta vikiwa katika hatua za mwisho za ujenzi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindiko, amepongeza jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu na maendeleo kwa ujumla.

"Ninawapongeza sana kwa ushirikiano wenu mzuri. Mmesimamia vyema ujenzi huu. Hii inaonesha namna gani Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha sekta ya elimu," amesema Mrindiko.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa ujenzi wa vyoo unapaswa kukamilika haraka ili wanafunzi 102 waliopangiwa kuanza masomo wasikumbwe na changamoto za miundombinu duni.

Aidha, amewataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kumuunga mkono Rais Samia na mgombea mwenza wake Dkt. Emmanuel Nchimbi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, akisisitiza kuwa chama hicho kiko imara na tayari kwa ushindani wa uchaguzi huo.

Kwa upande wao, wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bwana Daniel Kapaya na Giti Boniphace, wametoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao kwa njia bora, kuwapeleka shule, kanisani, na msikitini, pamoja na kuwafundisha kazi za mikono huku wakisisitiza kuwaepusha na vitendo vya ukatili.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi, Mhandisi James Jumbe, amesema wakati huu unahitaji zaidi uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mgombea mwenza wake, Dkt. Emmanuel Nchimbi, kutokana na uwezo wao wa kuwaletea Watanzania maendeleo.

Jumbe amempongeza Rais Dkt. Samia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta ya elimu, afya, na miundombinu, akisema hatua hiyo inaendelea kuleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa Shinyanga na Tanzania kwa ujumla.

Aidha, amesema uteuzi wa Dkt. Nchimbi kuwa mgombea mwenza wa Dkt. Samia ni ishara ya imani kubwa aliyonayo ndani ya chama na Taifa, akiwataka wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuwaunga mkono katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ziara ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini inaendelea, lengo likiwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia hali ya uhai wa chama, na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika kata zote za Jimbo la Shinyanga Mjini.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini Mzee Fue Mrindiko, akizungumza katika kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi, Mhandisi James Jumbe, akizungumza katika kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga Februari 19, 2025.



Post a Comment

Previous Post Next Post