" JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YATEMBELEA MIRADI CHIBE, NDEMBEZI NA IBINZAMATA WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YATEMBELEA MIRADI CHIBE, NDEMBEZI NA IBINZAMATA WANANCHI WAIPONGEZA SERIKALI

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini imewaomba wanachama na wananchi kuendelea kuweka imani juu ya CCM katika utatuzi wa kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Hayo yamezungumzwa na mwenyekiti wa jumuiya hiyo Mzee Fue Mrindoko pamoja na wajumbe wa kamati ya utekelezaji wa jumuiya hiyo wakati wa ziara yao ambapo leo Februari 20, 2025 jumuiya hiyo imefanya ziara katika kata ya Ndembezi, Chibe pamoja na kata ya Ibinzamata.

Ambapo katika kata ya Chibe wametembelea daraja jipya linalounganisha Chibe na kata ya Old Shinyanga ambapo kata ya Ibinzamata wametembelea mradi wa daraja la makabulini ambayo yote utekelezaji wake unaendelea vizuri huku wakimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utatuzi wa changamoto katika maeneo hayo.

Mrindoko pia ameipongeza serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa miradi ya maendeleo, ikiwemo miradi ya barabara, elimu, maji, na afya, na kuhimiza jamii kuendelea kushirikiana kwa pamoja katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Viongozi hao wamewahimiza wanachama wa CCM na wananchi kwa ujumla kuendelea kukiamini Chama cha Mapinduzi na kwamba changamoto zilizopo zitaendelea kuwekwa kwenye mpango ili kutatuliwa kwa mujibu wa Ilani ya chama hicho.

Kwa upande wake, Mjumbe wa kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, amesema ujenzi wa daraja kubwa la Chibe ni sehemu ya kazi nzuri zinazofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha miundombinu ya barabara inakuwa mizuri ili kuwezesha kukua kwa uchumi.

“Daraja la Chibe ni kubwa na zuri. Haya ni mambo mazuri yanayofanywa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan. Mama Samia ametekeleza Ilani ya CCM kwa zaidi ya asilimia 100. Ameonesha maendeleo ya kiuchumi kwa vitendo, nasi hatuna zawadi ya kumpa zaidi ya kumpatia kura za kutosha kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2025 kwa sababu tayari Chama kimempitisha kuwa mgombea Urais kupitia CCM pamoja na mgombea mwenza Dkt. Emmanuel Nchimbi ili waweze kutuletea maendeleo zaidi,” amesema Jumbe.

“Tunazo sababu nyingi za kutamba na Mama Samia, tunazo sababu lukuki za kumuunga mkono Rais Samia kwa mambo makubwa na mazito aliyoyafanya katika taifa hili. Amefanya mabadiliko makubwa katika mahusiano ya kimataifa, ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya, elimu, maji, umeme na kuimarisha demokrasia katika nchi ambapo hata vyama vya upinzani vinafanya mikutano yake kwa amani,” ameongeza Jumbe.

Jumbe ametumia fursa hiyo kuwaomba Watanzania kuendelea kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwakaribisha waliopo katika vyama vya upinzani na wasio na chama kujiunga CCM kwani ni chama imara chenye nia ya dhati ya kuwaletea maendeleo wananchi.

“Mwaka 2020 Shinyanga tulikuwa wa pili katika kukipigia kura kwa kishindo Chama Cha Mapinduzi, mwaka huu 2025 tunataka tushike nafasi ya kwanza. Nafasi ya Urais tayari tuna mgombea Mama yetu Mhe. Samia Suluhu Hassan, nafasi za Udiwani na Ubunge wagombea watapatikana kwa mujibu wa taratibu za Chama,” ameongeza Jumbe.

Diwani wa kata ya Chibe, Mhe. John Kisandu, amesema ujenzi wa daraja la Chibe – Old Shinyanga lenye urefu wa mita 45 linalojumuisha barabara, kalvati na daraja likigharimu jumla ya shilingi milioni 475, umekamilika na lipo katika matazamio huku akiomba taa ziwekwe katika eneo hilo ili kuimarisha usalama wapitaji kwani linatumiwa na watu kutoka maeneo mengi, ikiwemo kutoka Mkoani Tabora.

“Daraja hili limerahisisha mawasiliano kati ya kata ya Chibe na Old Shinyanga, kwa sababu hapa palikuwa hapapitiki wakati wa masika kutokana na kuwepo kwa mto mkubwa. Usalama sasa upo na mapato ya halmashauri yameongezeka kutokana na kwamba sasa wafanyabiashara wengi wanaokwenda katika mnada wa Old Shinyanga na Tinde wanapita katika daraja hili,” ameeleza Kisandu.

Naye Diwani wa kata ya Ibinzamata, Mhe. Ezekiel Sabo, amesema ujenzi wa Daraja la Ibinzamata Makaburini linasaidia kurahisisha kufika katika eneo la makaburini na maeneo ya jirani kwani eneo hilo lilikuwa halipitiki wakati wa masika baada ya daraja la awali kuvunjika.

Wananchi wa maeneo husika wameishukuru serikali kwa kujenga madaraja hayo ambayo yamerahisisha usafiri na kuondoa adha ya kutopitika kwa baadhi ya barabara wakati wa mvua ambapo wamesema madaraja hayo yamekuwa mkombozi kwao, hasa wafanyabiashara na wakazi wanaotumia njia hizo kila siku kwa shughuli zao za kiuchumi.

Jumuiya ya Wazazi Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini inaendelea na ziara ya kutembelea kata za Jimbo la Shinyanga Mjini, lengo kuu ni kuzungumza na wanachama na viongozi wa CCM, kufanya tathmini ya utekelezaji wa Ilani ya CCM, kuangalia hali ya uhai wa chama, na kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa katika maeneo hayo.

Wakiwa katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, amesisitiza umuhimu wa wanachama wa CCM kudumisha mshikamano na umoja ili kuimarisha chama na kuendelea na utekelezaji wa mipango yake ya maendeleo.

Naye, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mary Makamba, ametoa onyo kwa akina mama kuhusu madhara ya ulevi kwa familia.

Makamba amesisitiza kwamba ulevi, hasa pombe, unachangia migogoro ya familia na hata kudhoofisha afya ya akili ya akina baba ambapo ameeleza kwamba baadhi ya ndoa zimevunjika au kuingia matatizoni kwa sababu ya tabia ya wanawake kujiingiza katika ulevi.

Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Shinyanga Mjini Bwana Daniel Kapaya ametoa wito kwa jamii kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili, huku akionya kuhusu vitendo vya ulawiti na ubakaji, na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za haraka ili kukomesha vitendo hivi vinavyohatarisha usalama wa watoto.

Wakati huo huo Kapaya amewasisitiza wazazi na walezi kuwaepusha watoto na matumizi ya simu janja na kwamba hatua hiyo imekuwa ikisababisha mmomonyoko wa maadili na vitendo vya ukatili.

Naye mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Giti Boniphace, amewahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wanapata haki yao ya elimu huku akiwasisitiza kutimiza wajibu wao katika huduma stahiki.

Ziara hii inaendelea kuhamasisha umoja, maendeleo, na maadili mema katika jamii, huku wakazi wa Shinyanga Mjini wakiwa na nafasi ya kujadili masuala ya kijamii, kisiasa, na kiuchumi kwa lengo la kujenga mustakabali bora kwa wote.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mzee Fue Mrindoko, akizungumza na wanachama wa CCM, viongozi wa chama na jumuiya zake katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Februari 20, 2025.

Mjumbe wa kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, akizungumza na wanachama wa CCM, viongozi wa chama na jumuiya zake katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Februari 20, 2025.Mjumbe wa kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, akizungumza na wanachama wa CCM, viongozi wa chama na jumuiya zake katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga Februari 20, 2025.

Wanachama wa CCM, viongozi wa chama na jumuiya zake katika kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.


Katibu Elimu na Malezi jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Richard Mseti akizungumza katika kata ya Ndembezi.


Post a Comment

Previous Post Next Post