" JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YATEMBELEA KATA YA MASEKELO, NDALA NA MWAWAZA YAHIMIZA UMOJA KUELEKEA UCHAGUZI 2025

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YATEMBELEA KATA YA MASEKELO, NDALA NA MWAWAZA YAHIMIZA UMOJA KUELEKEA UCHAGUZI 2025

Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imewahimiza viongozi na wanachama wa chama hicho kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, utakaohusisha nafasi ya Rais wa Nchi, Wabunge na Madiwani.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Mzee Fue Mrindoko, pamoja na Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi inayotekelezwa chini ya Ilani ya CCM.

Ziara hiyo imefanyika Februari 21, 2025 katika kata za Masekelo, Ndala na Mwawaza zilizopo Jimbo la Uchaguzi Shinyanga Mjini.

Mrindoko amesema kuwa ili chama hicho kipate ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao, ni muhimu kwa wanachama kudumisha mshikamano na kuepuka makundi yasiyo na tija ndani ya chama.

Aidha, Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuimarisha maendeleo ya nchi huku akimhakikishia ushindi wa kishindo yeye pamoja na mgombea mwenza, Dkt. Emmanuel Nchimbi.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi, amewahimiza wanachama kutoridhika na idadi ya wanachama waliopo bali waendelee kuhamasisha wengine kujiunga.

"Tusiridhike na wanachama tulionao, naomba tuendelee kuongeza wanachama wapya. Wanachama hawa wasajiliwe kwa mfumo wa kielektroniki na tulipie ada za kadi zetu," amesema Bi. Kibabi.

Aidha, amekumbusha umuhimu wa kuendesha vikao vya kikatiba na kikanuni ili kuimarisha chama badala ya kushughulikia migogoro isiyo na tija.

“Tukumbuke kuwa uhai wa chama ni kufanya vikao. Fanyeni vikao vya kikatiba na kikanuni kwenye jumuiya zenu kwa sababu vikao vinajenga. Hali kadhalika, viongozi mliochaguliwa naomba muongoze kama inavyotakiwa, msifanye vikao vya kushughulikia watu, fanyeni vikao vya kujenga chama,” amesema Kibabi.

Katika ziara hiyo, viongozi wa jumuiya wametembelea ujenzi wa maboma mawili ya shule ya msingi Msufini B iliyopo katika mtaa wa Mlepa, kata ya Ndala, ikiwa ni sehemu ya juhudi za CCM katika kuimarisha miundombinu ya elimu.

Ziara hiyo inaendelea kuwa sehemu ya juhudi za CCM katika kuimarisha chama na maendeleo ya kijamii kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Ndala, Masekelo na MwawazaKatibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Bi. Doris Kibabi akizungumza wakati wa ziara ya Wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini katika kata za Ndala, Masekelo na Mwawaza

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, akizungumza katika wa ziara katika kata ya Masekelo, Ndala na Mwawaza.

 



 

Post a Comment

Previous Post Next Post