" JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAHIMIZA WANANCHI KUCHANGAMKIA MIKOPO YA ASILIMIA 10

JUMUIYA YA WAZAZI CCM WILAYA YA SHINYANGA MJINI YAHIMIZA WANANCHI KUCHANGAMKIA MIKOPO YA ASILIMIA 10

Na Mapuli Kitina Misalaba

Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini imewahimiza wakazi wa Manispaa ya Shinyanga kutumia vyema fursa za mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Akizungumza katika ziara ya jumuiya hiyo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Fue Mrindoko, amewasisitiza wananchi hususan vijana kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo hiyo ili kuimarisha maendeleo yao kiuchumi.

Ameeleza kuwa mikopo hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi kujiajiri na kupunguza changamoto za ajira.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha huduma za jamii na kutoa fursa za kiuchumi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na mikopo hiyo.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini, Bi. Doris Yotham Kibabi, amesisitiza umuhimu wa kuongeza wanachama wapya ndani ya CCM, akisema kuwa chama kinahitaji nguvu mpya na watu wenye ari ya kuchangia maendeleo.

“Tunahamasisha wanachama wapya kujiunga na Jumuiya ya Wazazi ili kushiriki katika shughuli za maendeleo na kujifunza masuala muhimu ya kijamii, ikiwemo malezi bora na ujenzi wa familia imara,” amesema Doris.

Naye Diwani wa Kata ya Chamaguha ambaye pia ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, amesisitiza umuhimu wa mikopo hiyo kwa maendeleo ya vijana, akiwataka kujipanga na kuunda vikundi vyenye malengo mahsusi ili waweze kunufaika na fursa hiyo.

Ameongeza kuwa Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, afya, elimu na maji, hivyo ni jukumu la wananchi kushirikiana kwa karibu na Serikali ili kunufaika na juhudi hizo.

Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini imehitimisha ziara yake ya kutembelea kila kata ndani ya Manispaa ya Shinyanga, ambapo leo wamefika katika Kata ya Kolandoto, Ibadakuli na Chamaguha.

Katika ziara hiyo, viongozi hao wametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika kata hizo, huku wakihimiza uzalendo, mshikamano na kuendelea kuiunga mkono CCM kwa kazi inayofanywa katika kuboresha maisha ya wananchi.

Ziara hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama akiwemo Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mhandisi James Jumbe, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya hiyo, Bi. Doris Yotham Kibabi, pamoja na wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini ambao ni Daniel Kapaya, Mwalimu Giti Boniphace, Mary Makamba, Zulfa Hassan pamoja na Katibu wa Elimu na Malezi wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Mzee Richard Mseti.

Aidha, jumuiya hiyo imetoa elimu kuhusu lishe bora, malezi, ukatili wa kijinsia na umuhimu wa wanachama wapya kujisajili ndani ya CCM.

Baadhi ya wanachama walioshiriki katika ziara hiyo wamepongeza juhudi za Jumuiya ya Wazazi kwa kutoa elimu juu ya masuala ya lishe, malezi na ukatili wa kijinsia, wakisema kuwa elimu hiyo itasaidia katika kuboresha maisha yao ya kila siku.

Ziara hii ni muendelezo wa juhudi za jumuiya hiyo katika kufuatilia na kushirikiana na wananchi katika miradi ya maendeleo, huku ikisisitiza ushirikiano wa karibu kati ya wananchi na Serikali katika kutimiza malengo ya maendeleo ya jamii ambapo wananchi wametakiwa kuchangamkia fursa zilizopo na kuendelea kudumisha mshikamano kwa ajili ya maendeleo endelevu.Viongozi mbalimbali baada ya kuwasili katika kata ya Kolandoto.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Ndg. Fue Mrindoko (wa pili kushoto), akizindua Shina la Wakereketwa la Wajasiriamali katika tawi la Chamaguha, kata ya Chamaguha

 

Post a Comment

Previous Post Next Post