Naibu Waziri Ofisi ya waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Patrobas Katambi amesema sheria za mifuko ya hifadhi ya jamii imetoa haki ya mwanachama kulipwa fidia endapo atacheleweshewa kulipwa mafao yake ikiwa ucheleweshaji huo umesababishwa na Mfuko.
Mhe. Katambi ameyasema hayo leo Februari 4, 2025 Bungeni, jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Fakharia Khamis ambaye alitaka kujua mstaafu aliyecheleweshewa kupata mafao anaweza kudai fedha kutokana na usumbufu alioupata wakati anasubiri mafao yake.
Amebainisha kuwa, vifungu 49(3) na 43(3) vinaeleza iwapo Mfuko utachelewesha kulipa mafao kwa mwanachama au uchelewesho huo haukusababishwa na mwanachama mwenyewe au mwajiri, Mfuko utamlipa mwanachama mafao yake pamoja na riba ya asilimia 15 kwa mwaka kulingana na kiasi atakachokuwa amelipwa kama mafao kwa Mfuko wa NSSF na asilimia 5 kwa Mfuko wa PSSSF.
Vile vile, Mhe. Katambi amesema Serikali imefanya mabadiliko ya sheria ya mafao ambapo wastaafu wanalipwa ndani ya siku 60, pia amesema mifuko ya hifadhi ya jamii imeboresha mifumo ya TEHAMA ambayo kwa sasa inamwezesha mwanachama kuangalia taarifa zake kupitia simu janja.
MWISHO