" KATIBU TAWALA WA MKOA WA SHINYANGA AISISITIZA BODI YA USHAURI YA HOSPITALI YA RUFAA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WELEDI

KATIBU TAWALA WA MKOA WA SHINYANGA AISISITIZA BODI YA USHAURI YA HOSPITALI YA RUFAA KUTEKELEZA MAJUKUMU KWA WELEDI

Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni akizundua Bodi Mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga leo Februari 11, 2025.

Na Mapuli Kitina Misalaba

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamdui, ameisisitiza Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kutekeleza majukumu yake kwa weledi, ikiwemo kuisimamia menejimenti ya hospitali katika utekelezaji wa majukumu yake.

Amebainisha kuwa menejimenti hiyo inawajibika moja kwa moja kwa bodi, huku Mganga Mfawidhi wa hospitali akihudumu kama Katibu wa Bodi.

CP Hamdui ametoa wito huo leo Februari 11, 2025, wakati akizindua rasmi bodi hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga na kwamba hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Vigmark Hotel, ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali na wadau wa sekta ya afya.

Hamdui amesema bodi inapaswa kukutana mara nne kwa mwaka, kila mwisho wa robo ya mwaka, ili kupitia na kuidhinisha au kukataa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Hospitali ambapo pia bodi inaweza kuitisha mikutano ya dharura kushughulikia masuala yenye athari katika utoaji wa huduma.

Aidha, bodi inawajibika kupitia maombi ya marekebisho ya bei za huduma za afya kwa kushirikisha wadau na kuzingatia miongozo, sheria, kanuni, na taratibu za nchi kabla ya kuwasilisha mapendekezo kwa Waziri mwenye dhamana.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, akisoma hotuba iliyoandaliwa na Mkuu wa Mkoa, amewapongeza wajumbe wa bodi kwa kuteuliwa na Waziri mwenye dhamana ya Afya ambapo amesisitiza kuwa bodi hiyo ni chombo muhimu katika uendeshaji wa huduma za afya katika Hospitali za mikoa.

“Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ni kiungo muhimu kati ya wananchi na serikali yao katika kusimamia utoaji wa huduma bora za afya,” amesema Katibu Tawala wa Mkoa.

Ameeleza kuwa Sera ya Afya ya mwaka 2007, kipengele cha 8.2, pamoja na Mwongozo wa Usimamizi wa Shughuli za Afya katika ngazi za mkoa wa mwaka 2019, vinaeleza umuhimu wa bodi za ushauri za hospitali za rufaa katika kuhakikisha uwazi na ushirikishwaji wa jamii katika utoaji wa huduma za afya.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. Luzila John, ametoa taarifa kuhusu Hospitali hiyo, akieleza historia na maendeleo yake tangu ilipoanzishwa mwaka 1947 baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Amesema Hospitali hiyo ilipandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Mkoa mwaka 1974 na kutangazwa rasmi kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa mwaka 2010 ambapo tangu mwaka 2022, Hospitali imekuwa ikitoa huduma katika eneo jipya lililopo Kata ya Mwawaza.

Dkt. Luzila amesema Hospitali hiyo inatoa huduma mbalimbali kwa wagonjwa wa nje na ndani, ikiwa ni pamoja na huduma za kibingwa za afya ya akina mama, watoto, upasuaji, magonjwa ya ndani, na huduma za dharura.

Kwa mwaka uliopita, hospitali ilihudumia wagonjwa wa nje 58,319 na wagonjwa waliolazwa 6,787ambapo akinamama 1,421 walijifungua hospitalini hapo, huku 802 wakifanyiwa upasuaji.

Amebainisha kuwa Hospitali hiyo imeendelea kuboresha huduma zake kwa kushirikiana na madaktari bingwa pamoja na kutumia mfumo wa huduma mkoba ili kuwafikia wananchi kwa urahisi.

Dkt. Luzila ameainisha changamoto mbalimbali zinazoikabili hospitali hiyo, ikiwa ni pamoja na upungufu wa miundombinu ya majengo ili kutoa huduma zote zinazohitajika na ubovu wa barabara zinazoelekea Hospitalini, jambo linalosababisha usumbufu kwa wagonjwa, hasa wale mahututi na waliovunjika mifupa.

Ameomba serikali iendelee kusaidia katika ujenzi wa miundombinu na kuboresha huduma za afya, huku akitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya afya.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt. Yudas Ndungile, amesisitiza kuwa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii, na Lishe ya Mkoa ina jukumu la kusimamia na kuratibu huduma za afya.

Amesema Hospitali hiyo ina wataalamu wa afya wabobezi wanaosaidia kuhakikisha huduma za kibingwa zinapatikana kwa wananchi.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya ushauri ya Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt. John Majigwa, akizungumza kwa niaba ya bodi, amesema:

“Sisi kama bodi tunapenda kuahidi kuwa tutafanya kwa uwezo wetu, kwa nguvu zetu na kwa upendo ili tuweze kuinua huduma za afya katika mkoa wetu. Bodi hii itafanya kazi kwa ushirikiano na watumishi wote, ngazi ya jamii na mkoa kwa ujumla, kwa sababu lengo letu ni kusaidia kuinua huduma za afya katika mkoa wetu ili kila mmoja aweze kufaidika na huduma hizi.”amesema Dkt. Majigwa

Uzinduzi wa bodi hiyo unatarajiwa kusaidia kuboresha huduma za afya katika Mkoa wa Shinyanga kwa kuhakikisha usimamizi mzuri wa hospitali na kushirikisha jamii katika maamuzi yanayohusu huduma za afya.

Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni akizundua Bodi Mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga leo Februari 11, 2025.

Katibu tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP. Salum Hamduni akizundua Bodi Mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga leo Februari 11, 2025.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt.Yudas Ndugile akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dkt.Yudas Ndugile akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. 

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Dkt.Luzila John akizungumza kwenye uzinduzi wa Bodi mpya ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Februari 11, 2025.

Viongozi mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Februari 11, 2025.

Viongozi mbalimbali katika hafla ya uzinduzi wa Bodi ya Ushauri ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga Februari 11, 2025.


Post a Comment

Previous Post Next Post