

Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Juu ya Kijeshi Kunduchi, Meja Jenerali Suleiman Mzee akizungumza wakati akifunga mafunzo ya tano ya pamoja kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Marekani, yaliyofanyika kambi ya Msata Chalinze mkoani Pwani Februari 15, 2025.

Kaimu Balozi wa Marekani Andrew Lentz akizungumza wakati wakati wa ufungaji wa mafunzo hayo katika eneo la mafunzo kambi ya Msata Chalinze mkoani Pwani.

Meja Jenerali Craig Strong Mkurugenzi wa Kikosi cha Jeshi la Marekani kutoka jimbo la Nebraska akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo katika ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Marekani.
………………..
NA JOHN BUKUKU, PWANI
Mkuu wa Chuo cha Mafunzo ya Juu ya Kijeshi Kunduchi, Meja Jenerali Suleiman Mzee, amefunga mafunzo ya tano ya pamoja kati ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Marekani, yaliyofanyika katika Kambi ya Msata, wilayani Bagamoyo, mkoa wa Pwani. Mafunzo hayo yalilenga kubadilishana uzoefu katika masuala ya kijeshi.
Akizungumza leo Februari 15, 2025, wakati wa hafla ya kufunga mafunzo hayo, Meja Jenerali Mzee alisema kuwa mafunzo hayo yanawaandaa askari wa Tanzania kwa kuwajengea uelewa wa pamoja kuhusu mbinu mbalimbali za kijeshi na namna ya kukabiliana na changamoto za kiusalama.
Aidha, alibainisha kuwa ushirikiano kati ya JWTZ na Jeshi la Marekani utaendelea, huku akisisitiza kuwa iwapo kutakuwa na haja ya kushirikiana na majeshi mengine, JWTZ litafanya hivyo kwa lengo la kuboresha ujuzi wa askari wake.
“Mazoezi haya yakiachwa kwa muda mrefu bila kufanyika, askari wanaweza kusahau mbinu walizojifunza. Hivyo, wale waliopata mafunzo wanapaswa kuendelea kuyadumisha na kuyatumia ipasavyo ili wanaposhiriki mafunzo yajayo wawe na uelewa mpana zaidi,” alisema Meja Jenerali Mzee.
Kaimu Balozi wa Marekani Andrew Lentz amesema kwa zaidi ya miaka 25 Marekani imefanya kazi kwa karibu na vikosi vya kijeshi na usalama vya Tanzania kwa kutoa elimu ya kitaalamu kwa maafisa wa TPDF na kukabiliana na ugaidi kuhakikisha ulinzi na kusaidia shughuli za kimataifa za kulinda amani.
Kwa upande wake, Meja Jenerali Craig Strong Mkurugenzi wa Kikosi cha Jeshi la Marekani kutoka jimbo la Nebraska ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu kwa washiriki kwani yanawaongezea uzoefu na kuwawezesha kushirikiana kwa ufanisi katika operesheni mbalimbali za kijeshi hasa zile za kulinda amani na kupambana na ugaidi.








Post a Comment